Morogoro. Temba na simba wanaotoka Hifadhi ya Taifa Mikumi mkoani Morogoro wamevamia mashamba na makazi ya wananchi wa Wilaya ya Mvomelo na kuzua taharuki sambamba na kuharibu mazao.
Akizungumza leo Jumamosi Februari 15, 2020 katika kikao cha bajeti cha baraza la madiwani Wilaya ya Mvomelo Diwani wa Doma, Elimu Kisugulu amesema wanyamapori hao wamekuwa wakionekana kuanzia saa 10 jioni.
“Ni kama wananchi tunawalimia wanyama hawa kwa sababu wanaharibu mazao yetu, hata wananchi sasa wanaogopa kutembea jioni. Ikifika saa 10 kila mtu amejifungia nyumbani kwake,” amesema diwani huyo.
Amebainisha jitihada zinazofanywa na Serikali kuwadhibiti wanyama hao hazitoshi, sasa wananchi wanataka kuonana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla.
Amesema miaka ya nyuma kila kijiji kilichopakana na hifadhi kulikuwa na askari wa wanyamapori, kwamba kwa sasa askari wapo watatu katika wilaya nzima ya Mvomelo.
“Niombe kwa ridhaa yako na wajumbe tulipofikia tukamuone Kigwangalla pengine tunaweza kupata muafaka kinyume na hapo tutaendelea kuzika watu kila mwaka hapa tayari tumezika wakazi wa kijiji cha Mangae, Mahalaka na Mtipule,” amesema diwani huyo.
Pia Soma
- Master Jay ‘aogopa’ kuoa akikumbuka yaliyompata Stamina
- Kalemani: Wanaolazimisha wananchi kununua nguzo za umeme wakamatwe
- Mvua yaharibu miundombinu ya shule nne mkoani Lindi
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Jonas Van Zeeland amemuagiza mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Florent Kyombo kutekeleza maagizo na kuandaa taarifa ya jitihada zilizochukuliwa, walipokwama ili aweze kufahamu maeneo yanayohitaji msaada.