Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madiwani halmashauri nane Mtwara kusitishiwa huduma za NHIF

Madiwani Mtwara Nhif.png Madiwani halmashauri nane Mtwara kusitishiwa huduma za NHIF

Fri, 6 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umetangaza kwamba utasitisha huduma za matibabu kwa madiwani wa halmashauri nane za Mtwara kuanzia Oktoba 25, 2023 kutokana na kutolipwa madeni ya matibabu.

Mbali ya mfuko huo, taasisi nyingine za umma nazo zimezikalia kooni halmashauri zikidai Sh73. 7 milioni ambazo zimetokana na malimbikizo ya madeni.

Halmashauri zinazodaiwa ni Mji Nanyamba, Nanyumbu, Tandahimba, Newala Mji, Newala Vijijini, Masasi Mji, Masasi Vijijini na Manispaa ya Mtwara Mikindani.

Akizungumza katika kikao cha ushauri cha mkoa, Meneja wa NHIF, Mkoa wa Mtwara, Dk Adolf Kihampa amesema waajiri wanashindwa kulipa michango ya watumishi wao kwa wakati wakiwamo madiwani kinyume cha taratibu.

Halmashauri moja tu ya Mtwara ndiyo iliyoonekana kutokuwa na madeni.

Miongoni mwa taasisi nyingine za umma zinazozidai halmashauri hizo ni Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) ambalo Meneja Mkoa wa Mtwara, Rebule Maira amesema ni makubwa na viongozi wake wanapaswa kulipa.

“Hadi kufikia Septemba, 2023 NSSF inadai zaidi ya Sh3.3 bilioni madeni ambayo yameshindikana kulipwa licha ya kuweka makubaliano ya muda mrefu. Kushindwa kuwasilisha michango hiyo imekuwa changamoto kwa kuwa baadhi ya watumizi wanashindwa kutimiza wajibu wao.”

Taasisi nyingine ni Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ambao Meneja wa Mkoa wa Mtwara amesema malimbikizo ya michango sasa ni zaidi ya Sh3.5 bilioni.

“Kwa kiasi kikubwa tumeona kuwa elimu ya masuala ya mifuko ya hifdhi inapaswa kutolewa kutokama na uelewa kuwa mdogo lakini pia wapo waajiri wamekuwa wakiwasilisha majalada ya mafao yakiwa na nyaraka pungufu.”

Mdai mwingine ni Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA) na meneja wake Mkoa wa Mtwara, Frank Kabendwe amesema kuwa madeni ya muda mrefu yamekuwa yakidhoofisha utendaji kazi wa taasisi hiyo.

“Changamoto ya madeni ya muda mrefu ni kubwa. Baadhi ya taasisi zinaonyesha hadi Septemba 2023 zinadaiwa Sh36.8 milioni. Tunazitaka kulipa haraka iwezekanavyo ili wakala uweze kutekeleza mipango yake kwa ufanisi.”

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas ametaka madeni hayo yalipwe haraka ili kuondoa sintofahamu ya malipo.

“Ni vyema mkirudi kama yapo madeni mlipe ili msikumbane na hizo kadhia ndio maana katika ziara yangu ilinifanya nitoe elimu ya umuhimu wa kujaza vizuri fomu za afya ili tusikose hizo fedha,” amesema Kanali Abbas.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live