Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madiwani Rorya wapitisha Sh5.5 bilioni za barabara

Madiwani Pic Data Madiwani Rorya wapitisha Sh5.5 bilioni za barabara

Thu, 30 Dec 2021 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Baraza la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya mkoani Mara imepitisha rasimu ya bajeti ya Sh5.5 bilioni kwa ajili ya matengenzo na ukarabati wa barabara kwa mwaka wa fedha 2022/23.

Fedha hizo zinatarajiwa kufanya ukarabati na matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilomita 137 pamoja na ujenzi wa madaraja na makalavati 22 katika wilaya hiyo chini ya usimamizi wa Wakala wa Barabara za Vijijni na Mijini ( Tarura) wilayani humo.

Akiwasilisha rasimu hiyo kwenye kikao maalum cha baraza hilo, meneja wa Tarura wilaya ya Rorya, Abbasi Hussein amesema kuwa bajeti hiyo imeongezeka kutoka Sh3.1 bilioni ya bajeti mwaka wa fedha 2021/22.

Amesema kuwa endapo fedha hizo zitapitishwa na bunge lijalo la bajeti zitatumika katika kuboresha miundombinu ya barabara wilayani humo ikiwemo ujenzi wa daraja la mto Mori litakalogharimu Sh1 bilioni.

"Kuna madaraja matatu makubwa yapo kwenye bajeti hii na madaraja hayo ni daraja la mto Mori, Nyathorogo na Wamahi yamekuwa korofi kwa muda mrefu hivyo ujenzi wake utakuwa ni suluhisho la kudumu kwa wakazi wa maeneo husika" amesema Hussein

Wakijadili rasimu hiyo, madiwani wa halmashauri hiyo wamesema kuwa ongezeko hilo la bajeti litasaidia katika kufungua wilaya ya Rorya kiuchumi kutokana na wilaya kuwa na miundombinu mibovu ya barabara kwa muda mrefu.

Diwani wa kata ya Kirogo, Justine Nyoswede amesema kuwa amefarijika kuona barabara muhimu hasa zinazounganisha wilaya hiyo na maeneo muhimu ya uchumi kama vile maeneo ya ziwa Victoria kwenye uvuvi wa samami zikiwa zimehusishwa kwenye bajeti hiyo.

"Kuwepo kwa barabara kama hii ya Nyamagaro- Nyang'ombe, Sota- Mwaloni ni ishara kuwa uchumi wa Rorya utafunguka maana  sote tunajua hali ya barabara hizo kwa sasa  na umuhimu wa samaki kwa uchumi wa  wilaya yetu" amesema Nyoswede.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Gerald Ng'ong'a amesema kuwa kutokana na bajeti hiyo kuunganisha taasisi zote muhimu wilayani humo madiwani wote watakuwa tayari kutoa ushirikiano wakati wa utekelezaji wake ili wananchi waweze kunufaika.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz