Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madiwani Nanyamba wamkataa DED

Madiwani Nanyamba Madiwani Nanyamba wamkataa DED

Sat, 10 Feb 2024 Chanzo: Mwananchi

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mji wa Nanyamba mkoani hapa wamemkataa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Thomas Mwailafu wakidai kuwa hashirikiani na baraza hilo.

Hata hivyo, alipoulizwa kwa simu leo Februari 10, 2024 Mwailafu ambaye hakuwepo kwenye kikao hicho, amesema atatoa maelezo yake atakaporejea ofisini.

"Bahati mbaya sikuwepo kwenye baraza, kwa hiyo sijasikia hayo malalamiko na sijayapata vizuri. Pia siwezi jua chanzo chake mpaka nikifike ndio naweza kuelezea," amesema Mwailafu.

Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani robo ya pili kilichofanyika Februari 9, 2024 Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji Nanyamba, Jamal Kapembe amesema kuwa baada ya malalamiko ya madiwani walilazimika kufanya kikao na kujadili utendaji kazi wa Mwailafu.

Amesema katika kikao hicho baadhi ya madiwani wasema hawana haja ya kufanya naye kazi kwa kuwa hawapi ushirikiano, hali inayoweza kuwafelisha katika uchaguzi mkuu ujao.

“Katika kikao tulichokaa madiwani wote kwa umoja wao wamesema hawana haja ya kufanya kazi na mkurugenzi huyo kwa kuwa hawapi ushirikiano, ambapo wamemshauri na kukaa naye kirafiki lakini wameona kuna dalili ya kuwaangusha katika uchaguzi mkuu ujao," amesema Kapende.

Akizungumzia malalamiko hayo, Diwani wa kata ya Nitekela, Salumu Chihediwe amesema wamekuwa wakitoa maagizo kwa kiongozi huyo, likiwemo la malipo ya watumishi yaliyotakiwa kulipwa mwaka uliopita.

Naye Diwani wa Kata ya Mnima, Salum Tino amesema kuwa wanahitaji maelekezo ili kujua fedha zilipo ambazo ni zaidi ya Sh90 milioni.

“Yaani tunahitaji maelezo tena yawe kwa maandishi ili tunapoambiwa kuhusu fedha tunaziona, lakini hizi hazipo kwenye taarifa halafu tunapewa mdomoni sio sawa sisi ni wawakilishi wa wananchi.”

"Kwa kuwa mmesema hatuna mamlaka ya kumjadili Mkurugenzi tunaomba Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (Tamisemi) amchukue mkurugenzi wake sisi tuko kwa niaba ya wananchi hatumtaki,” amesema Tino.

Akijibu malalamiko ya madiwani hao, Mwanasheria wa halmashauri hiyo, Prosper Kisinini aliyemwakilisha mkurugenzi, amesema kuwa baraza hilo halina mamlaka ya kumjadili kiongozi huyo, kwani ni kinyume na taratibu na kanuni.

"Hapa lazima tujue Mkurugenzi mamlaka yake ya uwajibikaji ni Katibu Mkuu Tamisemi, sisi mamlaka yetu ni wakuu wa idara na watumishi wengine.”

“Hatuwezi kufanya hivyo, ni nje ya utaratibu na kanuni na haya maswali yanaibuka kwa kuwa hatujikiti wala hatutambui nini tunakuja kufanya kwenye baraza,” amesema Kisinini.

Chanzo: Mwananchi