Baadhi ya madiwani wa Manispaa ya Lindi wamehosji sababu ya Chuo cha Maendeleo ya wananchi Chilala chenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 300, kuwa na wanafunzi 195 tu.
Wakizungumza na Mwananchi leo Novemba 10 baadhi ya madiwani wamewataka wazazi kuwa na mwamko wa elimu kwa watoto wao.
Diwani wa kata ya Ng'apa, Mwanaidi Mbungo amewaomba wazazi wasiwakatie tamaa watoto wao wanapomaliza shule na kushindwa kuendelea na masomo na kuwahimiza kupelekwa katika chuo hicho.
"Lengo la Serikali kuweka kile chuo ni kuwapatia elimu watoto wetu, niwaombe wazazi wenzangu kuna watoto wanao maliza darasa la saba hawakuchaguliwa kwenda kidato cha kwanza tuwapeleke katika kile chuo watapata ujuzi wa aina mbali mbali ambao utakuwa mwanga wamaisha yao.
“Hata walio fika kidato cha nne na hawakuchaguliwa kuendelea tunaweza kuwapeleka pale wakapate ujuzi," amesema Mbungo.
Amesema wapo wasichana wanaorubuniwa na kupata ujauzito na hivyo kukatisha masomo, lakini bado wanayo fursa ya kupata mafunzo chuoni hapo.
"Viongozi wote kwa ujumla katika manispaa hii tunaomba wazazi wawapeleke watoto ambao hawata pata nafasi yakuendelea na masomo wasiwaache wakae tu nyumbani," amesema Mbungo.
Naye Diwani wa Kata ya Rutamba, Athumani Mmaije amesema ametumia vikao kuwahamasisha wazazi kuwapeleka watoto katika chuo hicho kwa miaka miwili mfululizo lakini matokeo yake ni madogo.
"Nimeshauri kamati ya uchumi, nimeshauri baraza kupitia ofisa elimu msingi, akae na wataalamu wake ili wale wanafunzi wanaopata alama D wachukuliwe kupelekwa kwenye kile chuo ni kwenye ngazi ya shule zetu wenyewe sio ule mtaala rasmi ilimradi wazazi wawapeleke," amesema.
Naye Meya wa manispaa ya Lindi Frank Magali amewaomba madiwani kutumia mikutano katika kata zao kuwahamasisha wazazi wawapeleke watoto katika chuo cha maendeleo ya wananchi Chilala.
"Chuo kile ni chetu Lindi hii niyetu vyuo vya maendeleo viko vingi kwenye maeneo mengi, nchi hii ni moja, watu wanaruhusiwa kutoka maeneo mbalimbali lakini bado haita leta raha unaenda Chilala sisi wenyewe hatupo kabisa,” amesema.
Miongoni mwa kozi zinazotolewa chuoni hapo ni pamoja na umeme wa nyumbani, ufundi wa magari, uashi, ushonaji wa nguo na useremala.
Akizungumzia upungufu wa wanafunzi, Mkuu wa chuo hicho, Karimu Ngunguni amesema mwamko mdogo wa elimu kwa wazazi na vijana ndiyo chanzo cha kukosa wanafunzi katika chuo hicho.
Ngunguni amesema kama chuo wanajitahidi kutoa matangazo kupitia vyombo vya habari, mikutano pamoja na kuwatumia maafisa ustawi lakini bado muamko upo chini.
“Kwa nini mtoto atoke Zanzibar, Tandahimba na maeneo mengine waje kupata elimu huo ni muamko tu wakupenda elimu.
"Kulikuwa na fursa ya vijana kutoka kwenye kaya masikini kutoka manispaa ya Lindi kupata elimu bure walichaguliwa vijana thelathini na moja wakafika kumi na nane tu," amesema Ngunguni.