Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe limemuagiza Mkurugenzi na menejimenti ya Halmashauri hiyo kupeleka taarifa ya mapato na matumizi ya Julai hadi Desemba 2021 baada ya kutoridhika na utendaji wa menejiment hiyo.
Azimio hilo lilitokana na hoja iliyotolea na Mbunge wa Jimbo hilo, Timotheo Mnzava ambaye alieleza kutoridhika na utendaji wa Halmashauri hiyo ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa viashiria vya ubadhirifu na kutokutii maagizo ya Baraza la Madiwani.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Sadiki Kalaghe akisoma maagizo ya kikao cha Baraza hilo, alisema menejimenti hiyo inapewa wiki mbili kupeleka taarifa ya miradi ambayo inalalamikiwa ikielezea hali ya matumizi katika miradi hiyo, changamoto na mikakati ya utatuzi.
Aliitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja Mradi wa Jengo la Utawala la Halmashauri hiyo, wodi tatu za Hospitali mpya ya Wilaya, ukamilishaji wa zahanati tatu na ujenzi wa vituo vya Afya vya Kerenge, Mkumbara na Mnyuzi.
Pia kikao hicho kilitoa siku tatu kwa Menejimeti kukailimisha ujenzi wa stendi ya Mabasi ya Mombo ambayo ujenzi wake umekuwa ukisuasua kwa muda mrefu.
Akizungumza katika kikao hicho, Mbunge wa Jimbo hilo, Timotheo Mnzava alisema kuwa kumekuwa na uzembe katika ukusanyaji mapato na matumizi ya fedha ambayo hayafuati kanuni katika Halmashauri hiyo.
Advertisement Alitishia kuchukua hatua kali ikiwa ni pamoja na kushtaki katika Chama na Ofisi ya Rais ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kama Baraza litashindwa kuchukua hatua kurekebisha hali hiyo.
“Halmashauri hii ni moja ya Halmashauri ambazo zinakwenda hovyo na siko tayari kuwa sehemu ya haya, nitasimamia ukweli hata kama utagharimu kuachia ngazii niko tayari,” alisema Mnzava
Akitaja baadhi ya mambo ambayo alisema yanakwenda hovyo, alitaja uhamishaji wa fedha na matumizi ya fedha bila kufuata kanuni kama kupata kibali cha Kamati ya Fedha, kutolewa fedha taslim (baadala ya banki) kwaajili ya fidia na wanufaika kutolipwa kwa zaidi ya miezi miwili bila kujulikana zilipo fedha hizo na matumizi ya fedha kabla hazijafikishwa benki.
Alitaja mifano kuwa ni pamoja na Sh300m ambazo alisema zilikusanywa na kutumika bila kufikishwa benki na Sh18 milioni ambazo zilitolewa katika fungu la Sh240 milioni ambazo zimeletwa kwa ajili Mpango wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha (KKK) bila kufuata kanuni.
Fedha hizo zilitolewa kuwapa vikundi vya kina mama na vijana ambavyo vilipaswa kupewa fedha kutokana na mikopo ya ndani.
“Uzembe umesababisha fedha zisipatikane kwa wakati ajili ya kuendeleza miradi hiyo muhimu kwa wanananchi,” alisema Mbunge huyo.
Akizunguza katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya hiyo, Basila Mwanukuzi alizungumzia udhaifu ambao umejitokeza wa Mkurugenzi na Menejimenti yake katika kusimamia utendaji wa Halmashauri hiyo na kusisitiza kuwa viongozi hauwezi kukaa pembeni bila kuchukua hatua.
“Kama hatukusimamia bado lawama zitaturudia. Kama tulishiriki lawama zitaturudia. Lazima tufanye mambo kwa umakini mkubwa,” alisema na kusisitiza kuwa uongozi una dhamana kubwa sana kuhakikisha kuwa mambo yanakwenda sawa