Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madini, tangawizi, vanila kupaisha uchumi wa Mkoa wa Kilimanjaro

6891980fad261d4ea790bfa6f26f44fb.png Madini, tangawizi, vanila kupaisha uchumi wa Mkoa wa Kilimanjaro

Thu, 4 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

JULAI Mosi, mwaka jana Benki ya Dunia, iliiorodhesha Tanzania kuingia katika uchumi wa kati ambapo kila mkoa ukajiwekea malengo ya kuimarisha shughuli zake za uzalishaji mali ili kujiimarisha zaidi kiuchumi.

Kati ya mambo ya kuzingatia katika kujiinua huko kiuchumi ni pamoja na kuboresha kilimo, kutangaza utalii, kutumia rasilimali zote muhimu vema ili kuchangia ukuaji huo wa kiuchumi kuanzia ngazi ya mkoa ili kuchangia uchumi wa taifa kwa ujumla.

Kati ya mikoa ambayo imeitikia na kutekeleza dhana nzima ya kujiimarisha kiuchumi ni pamoja na Mkoa wa Kilimanjaro ambapo mkuu wa mkoa huo, Anna Mghwira katika mazungumzo na HabariLeo anaainisha mikakati ya mkoa katika kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja na mkoa mzima kwa ujumla.

Anasema mkoa huo umeamua kuwekeza zaidi katika sekta ya madini ambayo ni miaka miwili tu iliyopita yamegunduliwa wilayani Same mkoani humo. Madini yaliyogunduliwa ni ya vito.

Anasema mkoa umefungua vituo vya kuuzia madini wilayani humo ambapo wananchi wakishachimba huenda kuuza huko moja kwa moja na ambapo mapato ya serikali yanapatikana pia kutokana na mauzo hayo.

Mghwira anasema, hatua hiyo imekuwa na faida kwa serikali ya mkoa kwa kuwa mauzo hayo yanayofanywa na wananchi kwenye vituo huchangia mapato na wananchi pia wanakuwa na uhakika wa kupata fedha ambazo zinazungushwa wilayani na mkoani hapo kwa njia mbalimbali.

Anasema mkoa umefanikisha kupatikana kwa vibali kuuza madini hayo mikoa mingine ambapo wachimbaji wanaweza sasa kuyasafirisha hadi kwenye masoko ya Dar es Salaam na kwengineko.

Hata hivyo anabainisha kuwa kwa kuwa madini hayo yanapatikana milimani kuna changamoto ya barabara kuwezesha uchimbwaji huo wa madini, pia anawataka wawekezaji zaidi kusaidia upatikanaji wa vifaa vya kuchimbia vya kisasa ili madini yachangie zaidi pato la taifa.

Anasema,” kwa kiasi kikubwa hilo eneo lina madini mengi, yaani utashangaa kuona mtu ana ndoo imejaa aina za madini mbalimbali na tena yenye viwango bora huku nyumbani akiwa na ndoo nyingine kama mbili hivi za madini, sasa huo ni utajiri ambao tunazidi kuwasihi kupeleka madini katika vituo vya kuuzia ili wapate mapato wao na kuchangia serikali pia kwa njia ya kodi.”

Mkuu huyo wa Mkoa pia anabainisha mchango wa Tangawizi katika kuchangia uchumi wa mkoa, anasema wilayani Same tangawizi imebadilisha maisha ya wakazi wengi kwa kuwa ni zao linalolimwa kwa wingi huku uwekezaji wake pia ukichangia maendeleo ya mkoa huo kwa ujumla.

Anasema wananchi wanalima na kuuza kwa wingi kwenye viwanda vya usindikaji wilayani huyo ambapo huko nako kuna ajira kubwa zaidi kwa Watanzania imetolewa.

Mghwira anaongeza kuwa wapo wakulima ambao wanaamua kuuza hadi nje ya Wilaya ya Same na wengine wakifungasha wenyewe na kuuza sehemu mbalimbali za nchi.

Anasema mkoa umekuwa ukipata faida kutokana na kodi mbalimbali kutoka kwa wawekezaji lakini pia hata ushuru ambao wakulima wamekuwa wakitoa kwa njia mbalimbali.

Lakini Mghwira anabainisha kuwa ujio wa zao la kahawa umekuwa ni neema kwa wakulima wa mkoani humo lakini pia kuna kiasi fulani ni changamoto kwa kilimo hicho.

Anasema kuwa wakulima wengi ambao wanalima kibiashara wameacha kulima kahawa na kukimbilia katika zao la vanila kutokana na utofauti mkubwa wa bei ya ununuzi ambapo vanila kilogramu moja ni Sh 70,000 wakati kahawa ni Sh 5,000.

Anasema kuwa pia kutokana na ujio wa zao la parachichi wakulima wengi pia walikimbilia kwenye zao hilo na kuachana na kahawa kwa kuwa ukuaji wa kahawa, parachichi na vanila wote ni kwa wakati mmoja ambao ni miaka mitano.

“Yaani utakuta mtu ameacha kulima kahawa shamba zima ameweka parachichi au vanila, ila kwa sasa tumejipanga kuwaelimisha zaidi umuhimu wa kahawa pia, najua kahawa ya Tanzania ni kati ya kahawa bora duniani, ile harufu yake inawavutia wengi zaidi na wapo ambao huko ulaya wananufaika na mnyororo wa thamani wa kahawa yetu huku sisi tukiona hailipi”, anasema.

Lakini kwa kuwa mkoa huo kwa sasa umejipanga kujiinua kiuchumi, anaona kuwa ni nafasi mwafaka kuwashinikiza mabalozi wanaowakilisha Tanzania nje ya nchi kuitangaza kahawa ya Tanzania hatua ambayo itaunufaisha mkoa wa Kilimanjaro pia.

Anasema, “Kunahitajika pia kuwepo kwa nguvu kubwa ya kuwatafuta wanunuzi wa bidhaa hii waje hapa Tanzania, ni kwa nini wakulima wamekuwa wakipenda kwenda kuuza kahawa Uganda, hapa utagundua kuwa wana soko linalopeleka kahawa hadi Marekani na kwen gineko duniani, sasa hawa wanunuzi waje kuichukua hapa Tanzania, Huko inakopitishwa kabla ya kufika kwa mnunuzi mkuu inachakachuliwa kwa kuchanganywa na nyingine kisha ndio inapelekwa sokoni, sasa wanunuzi wakitafutwa na kuja kuwekeza moja kwa moja nchini watapata kitu cha ukweli na wakulima watanufaika zaidi.”

Kuhusiana na fursa nyingine za uwekezaji mkoani humo, Mghwira anasema kuwa mkoa huo una mashamba makubwa mbalimbali yanayofaa kwa uwekezaji na mengine yameshaajiri watu zaidi ya 2,000.

Anagusia mashamba ya maua kuwa yana fursa nyingi ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi, anatolea mfano wa shamba la maua lililoajiri watu zaidi ya 800 mkoani humo.

Mkoa wa Kilimanjaro unasifika kwa ufugaji pia hasa ng’ombe, kwa sasa umepania kukuza mifugo ya kienyeji anasema kuwa nguvu imewekwa kwenye ufugaji huo ili kuongeza wigo zaidi wa bidhaa za nyama.

Ili uchumi wa mahali ukue inabidi ziwepo Taasisi za kifedha zenye uwezo wa kuwakopesha wafanyabiashara wakubwa, wadogo na wa kati.

Benki ya Ushirika ya Kilimanjaro KCBC imebainisha kuwa mkoa huo utakuwa kiuchumi haraka hasa kutokana na mkakati wa benki kuanza kukopesha vyama vya ushirika, wakulima, wafanyabiashara na hata mtu mmoja mmoja.

Meneja Mkuu wa wa KCBC, Godfrey Ng’urah anavitaka vyama vya ushirika na Watanzania kwa ujumla kujiunga na huduma za benki hiyo huku akisisitizia nia ya benki hiyo ya kuvifikia vyama vyote vya ushirika nchini ambavyo ni vya kahawa, korosho, pamba, katani, alizeti na ufuta.

Anasema, “Benki inaunga mkono harakati za serikali hii inayoongozwa na Rais John Magufuli katika kuhakikisha uchumi wa nchi unaimarika zaidi, na menejimenti imeona kuwa kati ya walengwa ni vyama vya ushirika hasa tumeshaanza na vya Kilimanjaro”.

Anasema kutokana na mkopo wake kuwa wa riba ya asilimia 14 unaoweza kulipwa hadi kwa miaka nane tayari wakazi wa Kilimanjaro wameshaanza kuchangamkia na hivyo kuwa kwenye mazingira mazuri zaidi kufanya uwekezaji.

Anasema, “Hizi fursa za Kilimanjaro si ngumu kwa Mtanzania kuwekeza kwa kuwa benki inawakopesha kisha inatoa elimu ya biashara iwe kwa mjasiriamali mmoja mmoja, makundi au hata wafanyabiashara wakubwa”

Anashauri Watanzania kupitia vikundi vya vikoba, Saccos na umoja mbalimbali wa wajasiriamali kuwekeza kwa kuchukua mikopo kutoka katika benki hiyo.

Anawahakikishia usalama wa benki hiyo kwa kusema kuwa imepewa mtaji wa Sh bilioni nane kutoka benki ya CRDB kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya utendaji na mifumo.

Naye Anna Mghwira anasema kuwa benki hiyo ni kati ya nguzo muhimu za uchumi wa mkoa huo kwa kuwa imekuwa ikitoa huduma bora ambazo zinawawezesha wajasiriamali kujiinua zaidi.

Chanzo: habarileo.co.tz