Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madereva wapimwa upya

19337 Pic+madereva TanzaniaWeb

Thu, 27 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Chuo cha Ufundi Stadi (Veta) mkoani Mbeya kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani humo kimeanza kuwapima madereva wote wenye leseni ili kuona kama wanastahili kuendesha magari au wanahitaji kurudi darasani ikiwa ni agizo la Serikali katika kukabiliana na ajali.

Juzi madereva zaidi ya 100 kutoka ndani na nje ya Mbeya walimiminika katika chuo hicho kwa ajili ya kufanyiwa usahili chini ya usimamizi wa askari wa ukaguzi wa magari, watahini wa madereva na wakufunzi wa Veta.

Mkuu wa Chuo cha Veta Mbeya, Hassan Kalima alisema kwa kushirikiana na polisi wameamua kutekeleza agizo la Serikali la kuhakikisha madereva wote wanahakikiwa hata kama wana leseni.

“Unaweza kuwa dereva na una leseni lakini uliingia darasani mwaka 1980 lazima tuwe tunakumbushana mara kwa mara ili dereva huyu aweze kukumbuka sheria za barabarani na kujua barabarani kuna watumiaji wengi kama watembea kwa miguu, waendesha baiskeli.”

“Kwa sasa madereva wote wanatakiwa kuingia darasani kwani kuna alama za barabarani ambazo zimeongezeka na nyingine za zamani zimefutwa kutokana na kupitwa na wakati na pia kujua sheria mpya za usalama barabarani,” alisema Kalima.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mbeya, Jumanne Nkwa alisema madereva wote wanaofika chuoni hapo kabla ya kuingia darasani kujifunza kwa nadharia wanapelekwa kwanza kwenye mafunzo kwa vitendo ya kuendesha gari.

Alisema katika mafunzo hayo dereva anaangaliwa namna ya uendeshaji wake ili kujua mafunzo ya darasani anayopaswa kuanza.

Alisema mbali na mkakati huo, lakini pia polisi mkoani hapa wameanzisha utaratibu wa magari kupita kwa zamu kwenye miteremko mikali ya Iwambi-Mbalizi, mlima Nyoka-Uyole, Igawilo na mlima wa barabara ya Chunya ili kuepusha ajali.

Ajali yaua mmoja, kujeruhi 43

Yonathan Kossam anaripoti kuwa, wakati Veta ikiendesha mafunzo hayo, imetokea ajali na kusababisha kifo cha mtu mmoja na wengine 43 kujeruhiwa baada ya basi walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kupinduka eneo la Igodima kata ya Iganzo.

Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Dk. Prosper Mashaka alisema walipokea mwili mmoja na majeruhi 43, baadhi wakiwa wamevunjika miguu na majeraha kichwani.

Kamanda Nkwama amethibitisha kutokea ajali hiyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz