Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madereva wa Dangote wapewa somo la usalama barabarani

88852 Pic+dangote Madereva wa Dangote wapewa somo la usalama barabarani

Tue, 17 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mtwara. Uongozi wa kiwanda cha saruji cha Dangote mkoani Mtwara nchini Tanzania kimeendelea kutoa elimu ya usalama barabarani kwa madereva wake kwa kushirikiana na jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani na wadau wengine wa bima ili kuwakumbusha wajibu wao wawapo barabarani.

Akizungumza jana Jumatatu Desemba 16, 2019 mkuu wa kitengo cha usafirishaji, Gerald Osagie alisema wana madereva zaidi ya 600 na utoaji wa elimu hiyo ni utaratibu wa kawaida unaolenga kuwakumbusha wajibu wao ili kuhakikisha wanakuwa salama pindi wawapo safarini.

“Kila baada ya robo mwaka tutakuwa tunakutana na madereva wetu lengo ni kuwakumbusha wajibu wao wawapo barabarani kwa sababu tunatamani kuona tunatoa huduma nzuri, hivyo na wao wanapokumbushwa wajibu wao na kuzingatia tutasaidia kupunguza au kumaliza ajali za barabarani na kutoa huduma nzuri,” alisema Osagie

Alisema anatamani kuona wanawake wengi wakiomba nafasi hizo kwani jinsia zote zinaruhusiwa kikubwa ni kuhakikisha wanakidhi vigezo na masharti yaliyowekwa ili kutekeleza wajibu wao tofauti na sasa ambapo wana idadi ndogo ya madereva wa kike.

Mrakibu wa polisi mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Mtwara, Nestory Didi alisema wanaendelea kutoa elimu hiyo kwa madereva wa makundi mbalimbali kupitia vyombo vya habari na semina za ana kwa ana ili kuhakikisha wanawakumbusha madereva wajibu wao ikiwemo kutii sheria bila shuruti.

Mmoja wa madereva, Hafidhi Mkwachu alisema sababu za baadhi ya magari kupata ajali kutokana na uchovu wa madereva kutokana na kutopumzika lakini pia ubovu wa magari.

“Ili kuhakikisha ajali zinapungua au kuisha cha kwanza sisi madereva tunatakiwa kuwa makini kwa sababu mtu anaweza kuendesha gari mpaka saa saba usiku, lakini pia ubovu wa magari ikitokea tunatoa taarifa labda gari ni mbovu basi tusikilizwe na lifanyiwe kazi kwa wakati kwa sababu unavyoendesha gari ndivyo unavyopata pesa, ukiliegesha muda mrefu kwa maana hiyo hufanyi kazi,” alisema Mkwachu

Kiwanda cha Dangote kilianzshwa Julai 14, 2010 kwa sasa kina wafanyakazi zaidi ya 2,000 wenye ajira za kudumu na ajira za muda ambapo kina uwezo wa kuzalisha saruji tani tatu milioni kwa mwaka.

Chanzo: mwananchi.co.tz