Madereva na Makondakta wa daladala mjini Njombe wameandamana hadi kwa Kamanda wa usalama barabarani mkoani Njombe kupinga utaratibu wa Taxi za Kusalaliza zinazotajwa kuwakwamisha katika shughuli zao.
Madereva hao wamefikia hatua hiyo kufuatia serikali kupiga marufuku taxi za kusalaliza lakini zimekuwa zikikaidi agizo hilo hali inayowafanya kushindwa kuendesha biashara zao katika kiwango kizuri.
Wakizungumza mbele ya Kamanda wa usalama barabarani Mkoa wa Njombe Maro chacha madereva na Makondakta hao wamesema kuwa imekuwa ikiwapa shida jinsi ya kutatua tatizo hilo kutokana na kupigwa marufuku kwa Taxi hizo lakini wamekuwa hawatekelezi na kuwayumbisha kiuchumi.
Kufuatia malalamiko hayo Kamanda Maro Chacha amewataka Madereva na Makondakta hao wa daladala kuhakikisha wanadhibiti tatizo hilo wao wenyewe kwa kuwakamata madereva wa taxi hizo na kuwafikisha kituoni,msako uliopokelewa kwa nguvu zote na madereva hao.
Baada ya agizo la Kamanda Chacha mwenyekiti wa Daladala mkoa wa Njombe bwana John Mkondola amepongeza hatua hiyo na kuwataka madereva hao kuhakikisha wanazingatia sheria za biashara ya daladala ikiwemo kuwataka kusimama kwenye kituo kwa dakika tano tu na kumpisha mwingine.
Msako huo tayari umeanza kazi kwa kuwakamata madereva wa Taxi hizo huku wakitakiwa kukamata na kumfikisha kituoni bila kumpiga wala kumnyanyasa.