Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madereva bodaboda watajwa chanzo cha ubakaji, ndoa za utotoni

17912 Pic+kisarawe TanzaniaWeb

Wed, 19 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kisarawe. Wadau wa maendeleo na ustawi wa jamii Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani wametaja moja ya sababu zinazochangia ubakaji na ndoa za utotoni wilayani humo Kisarawe ni madereva bodaboda.

Wakizungumza leo Septemba 18,2018 katika warsha ya wadau wa kutokomeza ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto iliyofanyika wilayani hapa,  wadau hao wamesema umbali wa shule unasababisha wanafunzi walaghaiwe na madereva bodaboda na kuishia kupata mimba au kubakwa.

Akizungumza katika warsha hiyo iliyoandaliwa na Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo amesema ushirikiano wa wadau ni muhimu katika kumaliza ukatili huo.

"Ndiyo maana tumefurahi kwa Tamwa kuja hapa kwa sababu wanalifahamu tatizo hili kwa upana. Lakini pia tumewapata wazee maarufu na viongozi wa dini na maofisa ustawi wa jamii pamoja na wanasheria. Nia yetu tupate suluhisho la tatizo hilo," amesema.

Amesema kesi nyingi hazifiki mwisho kwa sababu ya kukosekana kwa ushirikiano wa wanafamilia pindi kesi zinapofika mahakamani.

Mkurugenzi wa Tamwa, Eda Sanga amesema unyanyasaji wa  watoto unaleta simanzi na ndiyo maana chama hicho kinapaza sauti na kusema imetosha Sasa.

"Kwa kauli moja tunasema huu unyanyasaji, ukatili, utovu wa nidhamu, visasi, uonevu, dhuluma na ukiukwaji wa  haki za mtoto kiujumla utokomezwe na utokomee," amesema.

Amesema Tamwa inatekeleza mradi unaowezesha wanawake na kujenga usawa wa kijinsia katika Wilaya saba Tanzania bara.

Chanzo: mwananchi.co.tz