Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madereva bodaboda Katavi walia na trafiki

Sat, 20 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Katavi. Umoja  wa  waendesha pikipiki (bodaboda) Manispaa  ya  Mpanda wamelilalamikia Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama Barabarani kutokana na baadhi ya askari wake kukamata pikipiki bila makosa.

Wametoa kauli hiyo leo Ijumaa Oktoba 19, 2018 wakati wakizungumza katika kikao cha dharura kilichoitishwa na  viongozi na mlezi wa chama hicho kujadili changamoto  zinazowakabili.

Mwenyekiti wa waendesha bodaboda wa wilaya ya Katavi, Asajile Mwakabafu amesema baadhi ya askari polisi wasio na sare wamekuwa kero kwa waendesha pikipiki, akidai wanawakamata na kuwabambikia makosa.

Amesema pamoja na kuwakamata pasipo makosa ya msingi, wakati mwingine askari hao wanaziharibu pikipiki hizo.

“Polisi wa mkoa huu wa ajabu sana yaani ukiegesha pikipiki unaenda kununua bidhaa sokoni wanakata nyaya na kuziunganisha kisha kuondoka na pikipiki,” amesema.

“Hawajali iwe upo kituo cha mafuta, umekwenda dukani wao kazi yao ni kuvizia tu ili waondoke na pikipiki.”

Hata hivyo, Kamanda wa kikosi cha usalama  barabarani Mkoa  wa  Katavi, William Mwamasika amesema waendesha pikipiki wamekuwa na tabia ya kuwakimbia trafiki wenye sare kila wanapowasimamisha barabarani kwa ajili ya ukaguzi.

"Hawa waendesha pikipiki wakijua wana makosa mara nyingi hawasimami wanapotakiwa kufanya hivyo,” amesema Mwamasika.

“Hatuwezi kuvumilia uvunjifu wa sheria kwa hiyo tunatumia askari wasio na sare kuwakamata wale wenye makosa kama ya kugonga watu na wanaowakimbia askari wenye sare.”

Amesema waendesha bodaboda wanaokamatwa kimakosa wanapaswa kutoa taarifa kwa viongozi wa juu wa polisi kwa hatua zaidi.

Mlezi wa chama cha bodaboda mkoani hapa, Beda Katani amesema waendesha pikipiki hao wanapaswa kufuata kanuni na sheria za usalama barabarani.

Pia, amesema polisi wanapaswa kutumia busara wanapokuwa katika kamata kamata.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz