Wafugaji na Madereva Wilayani Igunga Mkoani Tabora, wametakiwa kuacha tabia ya kupitisha Ngombe na magari yenye uzito mkubwa katika barabara za Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA), ili kuepuka uharibifu.
Hayo, yamebainishwa na Meneja wa TARURA Wilaya ya Igunga, Mhandisi Constantine Ibengwe wakati akitoa taarifa ya utekelezaji ya robo tatu ya mwanzo wa mwaka wa fedha 2022/2023 katika kikao cha baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Igunga.
Amesema, chanzo cha barabara nyingi za vijijini kuharibika mapema hutokana na baadhi ya wafugaji kupitisha Mifugo na magari yenye uzito zaidi ya tani 30, kitendo ambacho ni kinyume na sheria namba 13 ya matumizi ya barabara.
Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga, Joseph Sambo, aliliambia baraza hilo kuwa Wilaya ya Igunga imetenga maeneo kwa ajili ya wafanyabiashara wa mbao na maeneo ya kushushia mizigo, kwa wafanyabiashara wa soko la kati.