Majengo chakavu ya shule ya Msingi Mkalapa, wilayani Masasi Mkoa wa Mtwara yaelezwa kuhatarisha maisha ya wanafunzi na walimu.
Shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1947 na mwaka 1990 iliingiliwa na mafuriko, wananchi kwa kushirikina na Serikali walijenga madarasa ya muda ya matofari ya saruji na kujengewa na udongo.
Licha ya uchakavu wa miundombinu shule hiyo yenye wanafunzi 422 imekuwa ikifanya vizuri kitaaluma tokea mwaka 2018 katika mitihani ya darasa la nne na saba ikiwa na majengo nane chakavu. chakavuuupiiiic
Mwaka 2018, watahiniwa 43 walifanya mtihani wa darasa la saba na asilimia 95 walifaulu na kuifanya shule hiyo kushika nafasi ya pili kiwilaya na 15 kimkoa.
Mwaka 2019, wanafunzi 63 walifanya mtihani wa darasa la saba na kati yao asilimia 97 walifaulu na kuifanya shule hiyo kushika nafasi ya tatu kiwilaya na 11 kimkoa.
Katika matokeo ya 2020, shule hiyo ilifaulisha asilimia 100 ya wanafunzi 42 waliofanya mtihani ya darasa la saba na kuiweka katika nafasi ya kwanza kiwilaya na kimkoa pia katika shule za Serikali.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Salum Kimicha amesema mwaka 2021 shule hiyo ilishika nafasi ya tatu kiwilaya na 43 kimkoa kwa kufaulisha asilimia 100 ya wanafunzi 44 waliofanya mtihani wa darasa la saba.
Katika matokeo ya darasa la nne mwaka 2018 shule hiyo ilifaulisha asilimia 87 ya wanafunzi wake huku mwaka 2019 ikifaulisha asilimia 99 ya wanafunzi 65 waliofanya mtihani.
Aidha mwaka mwaka 2020 na 2021 shule hiyo ilifaulisha asilimia mia moja ya wanafunzi waliofanya mitihani.
Kaimu Mkurugenzi wa ya wilaya ya Masasi, Masumbuko Mtesigwa amesema Serikali imeelekeza kupelekwa kwa taarifa za mahitaji ya shule za msingi za wilaya hiyo kwa ajili ya maboresho na shule hiyo ni moja wapo ya zilizoorodheshwa.
"Hata sisi halmashauri katika bajeti ya mwaka huu wa fedha 2022/2023 ulioanza Julai, tuna mpango wa kujenga madarasa mawili katika shule hii na matundu 12 ya vyoo," amesema Mtesigwa.
Mwalimu Kimicha amesema licha ya miundombinu shule hiyo pia inakabiliwa na uhaba wa matundu ya choo.
Mwanafunzi wa darasa la saba katika shule hiyo, Haruna Liumbo amewaomba wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia kuboresha miundombinu ya shule yao.