Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madaraja ya mawe yanavyoifungua Kigoma kiuchumi

7b49f26596b88e39365bbc6ef158937b Madaraja ya mawe yanavyoifungua Kigoma kiuchumi

Tue, 29 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

AKIWA katika kampeni zake mkoani Kigoma hivi karibuni, mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Tanzania, Dk John Magufuli alizungumzia mpango wa kujenga barabara kimataifa inayopita katika mkoa huo.

Rais Magufuli alisema serikali imetenga shilingi bilioni 402 zitakazotumika kuhakikisha kwamba mtu anayetoka Kigoma, anayekwenda Tabora au Dar es Salaam asikanyage vumbi, sawa na mtu anayekwenda Mwanza au anayekwenda Uganda.

Kwa muda mrefu, usafiri wa uhakika mkoani Kigoma kutoka maeneo ya mengine ya Tanzania kama Dar es Salaam (umbali wa km 1316) au Mwanza (km 830) hadi Arusha (km 1204) umekuwa ni kwa njia ya reli au ndege lakini sasa usafiri wa barabara pia unaelekea kuwa wa uhakika.

Bila shaka Rais Magufuli akichaguliwa tena na barabara hiyo kuzidi kuufungua zaidi mkoa huo wa mpakani, maisha ya wananchi wa Kigoma yatazidi kuwa mazuri zaidi na kuharakisha mkoa huo kuelekea kwenye Tanzania ya viwanda.

Hii inatokana na namna Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) unavyoendelea kuboresha barabara za mkoa huo wa Kigoma unaopakana na nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa kutenganishwa na Ziwa Tanganyika.

Kiuchumi, wananchi wengi wa mkoa wa Kigoma wanategemea kilimo, wakijihusisha katika kulima mazao mchanganyiko huku zao kuu la biashara ikiwa chikichi.

Mazao mengine yanayolimwa Kigoma ni miwa, nanasi, ndizi, maharage na muhogo ambao kwa miaka kadhaa sasa umekuwa na soko kubwa katika nchi jirani za Burundi na Rwanda. Kigoma pia ina hifadhi maarufu ya sokwe iliyoko Igombe.

Tarura inavyoimarisha barabara Mratibu wa Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (Tarura) mkoani Kigoma, Godwin Mpinzile anasema, wakala mkoani humo unaendeleza ujenzi wa barabara pamoja na madaraja ili kuzidi kuufungua mkoa huo.

Akizungumzia madaraja, Mpinzile anasema serikali imekuwa ikishirikiana na nchi ya Ubelgiji kupitia kampuni ya Enabel katika ujenzi wa madaraja kwa kutumia mawe.

Anasema hatua hiyo, licha ya kuokoa gharama lakini inazidi kuboresha barabara za mkoa huo wenye mito kadhaa na vijito na hivyo kuwezesha mazao ya wakulima kufika sokoni.

“Sisi Tarura tuna dhamana kubwa kuhakikisha tunatengeneza miundombinu thabiti ili kuwezesha shughuli za usafiri na usafirishaji wa mazao kutoka mahali pa uzalishaji hadi kwenye soko,” anasema Mpinzile.

Mratibu huyo anazungumzia kidogo zao la muhogo lililoanza kulimwa kwa wingi wilayani Kibondo mwaka 2009 na kuwa na umaarufu mkubwa wilayani humo na hatimaye kusambaa mkoa mzima.

Taarifa zinaonesha kwamba miaka ya 2010 nchi za Rwanda na Burundi zilikabiliwa na baa la njaa na hivyo muhogo ukapata soko kubwa katika nchi hizo na kusababisha wakulima wengi Kigoma kuligeukia zao hilo.

Maharage yanayolimwa Kigoma inaelezwa kwamba yamekuwa pia yakipata soko nchini Ubelgiji, hivyo juhudi za kuzidi kuufungua mkoa huo wenye ardhi yenye rutuba ni muhimu kwa wananchi wa Kigoma na taifa kwa ujumla.

Bosi huyo wa Tarura Kigoma anasema pamoja na mazao yanayolimwa Kigoma kuhitajika kwenye soko, tatizo kwa miaka mingi lilikuwa barabara za ndani na za kuunganisha mkoa, huku madaraja pia yakiwa tatizo kubwa.

Mradi wa madaraja ya mawe Meneja wa Tarura katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Abed Fundi, anasema Tarura kwa kushirikiana na Enabel waliwapa wananchi elimu juu ya mradi wa madaraja ya mawe na faida watakayopata baada ya kujengwa kwa madaraja hayo.

Kazi nyingine anasema ilikuwa ni kuwahamasisha wananchi kupitia serikali zao za vijiji kujitolea kukusanya mawe kwa ajili ya kujengea madaraja hayo pamoja na kujitolea kuwasaidia mafundi katika kuyajenga.

Fundi anasema teknolojia ya kutumia mawe kujenga madaraja ni imara na kwamba madaraja yanadumu sana kulinganisha na madaraja ya zege licha ya kwamba gharama zake ni nafuu pia.

Anatoa mfano kwamba daraja la kalavati la mita moja, kama utatumia mawe utahitajika tripu nane za mawe kwa gari ya tani saba gharama yote ya kulijenga daraja hilo ni shilingi milioni nne wakati kwa daraja la zege la namna hiyo gharama yake ni shilingi milioni 21.5.

“Daraja la mawe la mita nne ujenzi wake kwa kutumia mawe ni shilingi milioni 13, wakati lile la zege ni shilingi millioni 78, hivyo ukitumia mawe unaokoa takribani asilimia 83 ya fedha ambazo zingetumika,” anasema.

Mhandisi huyo anaendelea kusema kwamba Tarura hushiriki kwenye ujenzi wa barabara katika maeneo ya mradi wa madaraja hayo yaliyo chini Enebel huku wakitoa ushauri wa kitaalamu na usimamizi.

Anazidi kusisitiza kwamba ujenzi wa madaraja ya mawe una faida kubwa kwani yanakuwa imara, hukaa muda mrefu yanaweza kubeba uzito kati ya tani 15 hadi 40.

Lakini anasisitiza kwamba upatikanaji wa daraja unategemea utayari wa kujitolea wa wananchi au wanakijiji. “Isitoshe ushiriki wa wananchi unapelekea mafundi na jamii kupata ujuzi wa ujenzi wa madaraja ya mawe,” anasema Fundi.

Glory Mwanga, mwanakijiji katika kata ya Mkongoro anasema ujenzi wa daraja la Vyabigufa katika kata yao kwa kutumia mawe umekuwa ni mkombozi mkubwa wa wananchi wa kata hiyo.

“Tulikuwa tunapata shida sana hasa kipindi cha mvua, barabara ilikuwa haipitiki kutokana na kukosekana kwa daraja la uhakika. Watu wengi wa kata yetu wamekufa maji kati eneo hilo,” anasema.

Meneja Fundi anasema katika halmashauri hiyo ya Kigoma pia wamekuwa na mradi wa daraja la chuma kama kivuko cha watembea kwa miguu katika eneo linaloitwa Nkungwe.

Anasema daraja hilo limejengwa na Tarura kwa fedha za mfuko wa barabara na kugharimu shilingi milioni 212. Anasema hatua hiyo imewaokoa wananchi waliokuwa wakizolewa na maji ya mto au kuliwa kama si kujeruhiwa na mamba kutokana na mto huo kuwa na mamba wengi.

“Kabla ya ujenzi wa hilo daraja wananchi wa kata ya Nkungwe walikuwa wanapata tabu ya kuvuka ng’ambo ya pili kujipatia mahitaji muhimu.

Lakini shida pia ilikuwa kwa wanafunzi wanaosoma ng’ambo nyingine wakati wa kwenda shule pamoja na wakulima kwenda kwenye mashamba yao,” anasema.

Meneja wa Tarura katika halmashauri ya wilaya ya Kasulu, Shilungu Shija anasema Tarura kwa kushirikiana na Enabel wamepanga kujenga madaraja ya mawe matano.

Anasema wameshaanza kujenga madaraja matatu kwa mwaka huu wa fedha kwa ushirikiano na wananchi na kwamba madaraja mawili bado yapo kwenye mchakato wa kuanzwa kujengwa.

Anasema madaraja hayo ni muhimu sana kwa kuzingatia kwamba Kasulu ndio yenye wakulima wakubwa wa muhogo, maharage na migomba.

“Tumekusudia kumaliza kabisa changamoto ya miundombinu ya barabara kwa wananchi wa Halmashauri ya Kasulu ili waweze kusafiri na kusafirisha mazao yao kwa urahisi kabisa,” anasema Shilungu.

Madaraja ya mawe yanavyoifungua Kigoma kiuchumi Daraja

Chanzo: habarileo.co.tz