Moshi. Uwepo wa madalali katika kituo kikubwa cha mabasi Mjini Moshi mkoani Kilimanjaro umeelezwa kuwa chanzo cha upandishwaji nauli kiholela kwa magari yaendayo mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam.
Nauli halali kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiru wa Nchikavu na Majini (Sumatra) ni kati ya Sh28,5000 na Sh32,800 lakini madalali hao wamekuwa wakiuza tiketi kwa Sh35,000 hadi Sh40,000.
Wakizungumza na Mwananchi leo Jumatano Januari 2, 2019 baadhi ya abiria wamelalamika kupewa tiketi zenye kiwango cha Sh28,000 huku wakizilipia Sh32,000 na wengine wamedai kutozwa Sh35,000 hadi Sh40,000.
Hadija Juma ambaye ni miongoni mwa abiria wanaosafiri kwenda Dar es Salaam amesema amekata tiketi kwa Sh32,000 lakini tiketi aliyopewa imeandikwa Sh28,500.
"Nimekuja hapa asubuhi na mapema, nikapewa tiketi kwa Sh32,000 lakini ilikuwa imeandikwa Sh28,500 nilipoingia kwenye gari wakaja watu wakikagua walipohoji wale mawakala wakaagizwa wanirudishie hela yangu, wakanishusha kwa hasira," amesema Hadija.
Akizungumza ofisa mfawidhi Sumatra, mkoa wa Kilimanjaro, Johns Makwale amekiri kuwepo kwa tatizo la madalali na kuwataka abiria kukata tiketi kwenye ofisi za magari.
"Kila siku tumekuwa tukitoa tangazo kuwataka abiria kukata tiketi ofisi za magari husika ili kuepuka utapeli unaofanywa na madalali, la sivyo wataendelea kulanguliwa na kuitupia lawama Sumatra," amesema Makwale.