Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madaktari watuhumiwa kulewa wakiwa kazini

Peter Serukamba.png Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba.

Mon, 23 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wananchi wanaokwenda kupata huduma za matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Manyoni mkoani Singida, wamedai baadhi ya madaktari hukwenda kazini wakiwa wamelewa na kushindwa kuhudumia wagonjwa.

Walimlalamikia Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, kwenye kikao cha kusikiliza kero wilayani Manyoni.

"Januari 4, mwaka huu saa 3:00 usiku nilimpeleka mtoto wangu katika Hospitali ya Wilaya ya Manyoni ambaye alikuwa ameumia kidole, nikamkuta daktari mmoja ambaye alikuwa amelewa chakali na kushindwa kumhudumia kabisa mgonjwa kwani alikuwa hajiwezi," alidai Prisca Maleta.

Alidai katika hali ya kushangaza, daktari huyo mlevi aliwaambia kama wapo jirani wachukue vifaa vya matibabu wakavifanyie usafi na kisha wamsafishe jeraha (kidonda) mgonjwa na kumwekea dawa.

Maleta alisema baada ya kuambiwa hivyo na daktari huyo alilazimika kumchukua mtoto wake saa nane usiku na kumpeleka katika hospitali binafsi eneo la sokoni Manyoni ambako alipatiwa huduma ya kwanza.

Maleta, alisema siku iliyofuata alimpeleka mtoto wake kupata matibabu katika Hospitali ya St. Gasper inayomilikiwa na Kanisa Katoliki iliyoko Halmashauri ya Itigi.

Alimwomba Mkuu wa Mkoa Singida, Serukamba awasaidiwe kuondolewa kero hizo kwa sababu wananchi wengi wanaathiriwa na hali hiyo katika Hospitali ya Wilaya ya Manyoni kutokana na matukio ya baadhi ya madaktari kwenda kazini wakiwa wamelewa yamekuwa yakijitokeza mara nyingi.

Kutokana na kero hiyo, Serukamba, aliagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani Manyoni, kuchunguza utendaji wa watumishi wakiwamo madaktari katika hospitali hiyo na apelekewe taarifa ya uchunguzi huo Ijumaa, wiki hii.

Alisema utaratibu huo wa kukutana na wananchi, kusikiliza kero zao na kuzipatia utatuzi papo hapo ni endelevu na atakutana na wananchi katika kila wilaya mara moja kwa mwezi.

Malalamiko yaliyotawala ni migogoro ya ardhi na uamuzi ulifikiwa kwamba Kamishna wa Ardhi Msaidizi wa Mkoa Singida, Shamim Hoza, ashirikiane na watumishi wa ardhi wa wilaya hiyo kupitia migogoro yote ya viwanja na watoe mapendekezo kuhusu njia zinazoweza kuimaliza zikiwamo za maridhiano.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Manyoni, Fadhili Chimsala, aliagizwa kushirikiana na watendaji wake kuorodhesha migogoro yote ya umiliki wa mashamba na usafishaji wake, waite kila muhusika na kuzungumza nao mpaka wafikie maafikiano, yaandikwe na kutiwa saini na pande zote husika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live