Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

“Machozi na damu” ilivyodhibiti uvuvi wa mabomu Dar

30423 Uvuvipic Wavuvi wa Samaki

Thu, 6 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Pembezoni mwa Kijiji cha uvuvi cha Kizito Huonjwa katika mji mdogo wa Kimbiji takriban kilomita 40 kutoka katikati ya jiji la Dar es Salaam, pilikapilika za wavuvi na wafanyabiashara wa samaki zimetoweka.

Mtu anayefika kwa mara ya kwanza katika eneo hilo la Wilaya ya Kigamboni, hawezi kugundua haraka kuwa liliwahi kuwa soko kubwa la samaki kutokana na ukimya. Baadhi ya makazi ya familia za wavuvi yametelekezwa baada ya msako mkali uliofanywa na vyombo vya dola.

Ukimya umetokana na usitishwaji wa soko hilo la samaki baada ya Serikali kubaini lilikuwa ni moja ya vituo vikuu vya uvuvi haramu wa kutumia mabomu jijini hapa.

Maeneo mengine ambayo yalikuwa yakitumika kwa uvuvi haramu, kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na tovuti ya habari za uchambuzi ya Nukta, ni Kunduchi, Kawe na Ununio katika Halmashauri ya Wilaya Kinondoni; Buyuni na Minazi Mikinda (Kigamboni).

Hata hivyo, kwa sasa sehemu kubwa ya uvuvi wa mabomu umepungua baada ya operesheni kali ya baharini na nchi kavu iliyoendeshwa na Kikosi kazi cha kitaifa (Mult Agency Task Team - MATT).

Kikosi hicho kilichoundwa kuzuia uhalifu wa kimazingira na kusimamia uvuvi wa bahari kuu, kinajumuisha wataalamu kutoka JWTZ, Polisi, Usalama wa Taifa, maafisa uvuvi, mazingira, mashirika yasiyo ya kiserikali na wavuvi wa maeneo husika.

Operesheni ya ‘machozi na damu’

Operesheni kubwa iliyowaondoa wavuvi wengi haramu jijini hapa, ilianza Januari mwaka huu baada ya MATT kujumuisha mbinu mpya za msako wa baharini na nyumba kwa nyumba katika maeneo ya wavuvi hao ikiwemo Kizito Huonjwa.

Mmoja ya wavuvi waliokuwa wakijihusisha na uvuvi wa mabomu kabla ya kuachana nao hivi karibuni, Omary Mussa Omary anasema hajawahi kuona operesheni kali kama hiyo kwa kuwa ilizua taharuki kwa wavuvi na wakazi.

“Kwanza walikuja kwa siri wakataka kujua kina nani wanajihusisha na uvuvi huo na wanawapataje,” anasema Omary aliyepoteza kidole baada ya kulipukiwa na bomu wakati akivua samaki.

“Kwa sababu ya ile nguvu iliyotumika kuwakamata watuhumiwa…hadi wanawake nyumbani walikuwa wakiwaambia wanume zao ‘kama unafanya uvuvi wa bomu mimi sikutaki,” anasema Omary.

Selemani Kondo, mvuvi na mkazi wa Kizito Huonjwa, ilimbidi aitelekeze familia yake kwa zaidi ya wiki tatu akihofia kukamatwa kabla ya kujisalimisha ofisi za Serikali ya mtaa na kukubali masharti ya kuachana na uvuvi wa mabomu.

Mtafiti wa masuala ya bahari, Gill Braulik kutoka kampuni ya utafiti na uhifadhi ya Downstream (Downstream Research & Conservation) anasema kuwa mtandao wao wa ving’amuzi vya kurekodi sauti za mabomu katika ukanda wa pwani nchini, umeripoti millipuko kwa kiasi kidogo sana jambo linalosadifu kauli za jamii ya wavuvi kuwa uvuvi wa aina hiyo umepungua kwa kiwango kikubwa.

“MATT walitusaidia sana katika maeneo ambayo sisi hatukuweza kufika awali,” anasema Emmanuel Bulayi, Mkurugenzi wa Uvuvi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Doria hizo zilihusisha kuharibu na kuteketeteza mitumbwi na malighafi zote za kutengenezea mabomu ili kuhakikisha wahusika hawaendelei kuvua kwa njia zisizokubalika kisheria.

Baada ya operesheni hiyo, Bulayi anasema kuwa tathmini ya awali inaonyesha kwa sasa uvuvi wa kutumia mabomu katika ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi umekomeshwa kwa asilimia 85.

Wakati mkurugenzi huyo akieleza mafanikio hayo, vyanzo vyetu vimeeleza kuwa baadhi ya wavuvi wameanza kutumia mbinu mpya za uvuvi haramu ikiwemo milipuko isiyotoa sauti “silent bombs” ili kukwepa mkono wa sheria.

Mbinu hiyo inahofiwa na wataalamu wa viumbe vya baharini kuwa huenda inahusisha matumizi ya kemikali kama ‘chroline’ ambayo ni hatari kwa afya za binadamu na viumbe wengine wa majini.

“Pamoja na uvuvi wa mabomu kupungua, ving’amuzi vyetu vilivyopo baharini vimerekodi sauti mbalimbali katika ukanda wa pwani wa Tanzania. Japo utafiti unaendelea kuhusu jambo hilo lakini milipuko hiyo ya (chroline) inajulikana kama “mabomu ya kimyakimya” kwa kuwa haitoi sauti juu ya usawa wa maji,” anasema Braulik.

Lydia Mwakanema, Afisa Mradi wa Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi na Bahari katika Mfuko wa Wanyama Pori (WWF), anasema matumizi ya mabomu yasiyotoa sauti yanafanya iwe vigumu kwa vyombo vya dola na wale wanaosimamia sheria, kufuatilia na kujua mahali mlipuko ulipotokea.

Licha ya kuwa wanafuatilia suala la milipuko ya kimyakimya kupitia utafiti wa kina, Mwakanema anasema; “Taarifa za awali zinaonyesha kuwa wavuvi wanatengeneza milipuko mikubwa yenye ujazo wa ndoo ya lita 20 ambayo ikilipuka inaharibu mahali pakubwa”.

Mbinu nyingine iliyozuka baada ya uvuvi wa mabomu ni matumizi ya tochi zenye mwanga mkali ambazo wavuvi huzama nazo baharini ili kuwalevya samaki na kuwakamata kirahisi.

“Zile tochi sijui zina madini gani, samaki wakimulikwa wanalala kabisa, mvuvi anapata nafasi ya kuwachoma kirahisi,” anasema Omary. Hata hivyo, polisi wanaeleza kutobaini aina hiyo mpya ya uvuvi haramu hadi sasa.

“Kama kuna uvuvi wa mbinu hiyo watu watoe taarifa mapema ili mchakato ufanyike na kuwakamata wahusika,” anasema Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa.

Unavyowagharimu walipakodi

Vita dhidi ya uvuvi haramu huitaji rasilimali nyingi ikiwamo watu na fedha za umma ambazo zilipaswa kugharamia miradi ya maendeleo kama elimu, afya na maji.

“Gharama zilizotumika kwa operesheni nzima bajeti yake ilikuwa Sh89 milioni kwa mwaka na tunaendelea vizuri,” anasema Bulayi.

Hata hivyo, Bulayi katika mahojiano zaidi alieleza kuwa kiasi cha fedha za doria hutegemea kiwango cha uvuvi haramu. Nukta ilifanya uchunguzi na kubaini kuwa wavuvi haramu walikuwa wakivua kwa vilipuzi vya kisasa na vya kizamani bila kuhofia mamlaka za kisheria.

Serikali inasema kuwa katika operesheni hiyo ya MATT kwa kushirikiana na shirika la Sea Sense iliyofanywa kati ya Januari na Juni mwaka huu watuhumiwa 32 walikamatwa na kesi 13 zilifunguliwa mahakamani.

Mbali na kesi, wizara inasema faini ya Sh15.45 milioni zilikusanywa kutoka kwa waliotiwa hatiani.

Wadau wa uvuvi wanasema utashi wa kisiasa wa viongozi wa Serikali umesaidia operesheni ya kutokomeza uvuvi wa mabomu hasa baada ya Rais John Magufuli kuingia madarakani mwaka 2015 kutaka shughuli zote za uvuvi haramu zitokomezwe ili wananchi wafaidike na rasilimali za bahari na maziwa.

“Rais mwenyewe Julai 2016 alitoa hotuba kuonyesha kutokuwapo kwa uvumilivu katika uvuvi haramu, hivyo ni bora wadau wote tushirikiane kutokomeza uvuvi huo,” anasema Mkurugenzi wa Shirika la uhifadhi wa viumbe wa baharini la Sea Sense Tanzania.



Chanzo: mwananchi.co.tz