Machinjio ya kisasa kwa mifugo ya Nguru Hills Ranch Ltd yataanza kutumika Machi Mosi mwaka 2022.
Katika machinjio hayo yaliyopo wilayani Mvomero mkoani Morogoro kwa siku watakuwa wakichinjwa ng’ombe 100 na mbuzi 1,000 na kuchochea ukuaji wa uchumi na ajira.
Mradi wa machinjio hayo ya kisasa ni upo chini ya ubia wa Serikali kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF ), Eclipse Investiment (LLC) na kampuni ya Busara Investment (LLP).
Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji wa PSSSF , Fortunatus Magambo amesema hayo mbele ya wahariri wa vyombo vya habari waliotembelea mradi wa machinjio ya kisasa ya Nguru.
Amesema mradi huo ulianza mwaka 2018 lakini ugonjwa wa Uviko-19 ulipoanza ulisababisha mashine zilizoangizwa kutoka nje ya nchi kuchelewa kuwasili nchini wakiwemo na wataalamu wa kuzifunga hadi kufikia Julai 2021.
Amebainisha kuwa mifumo ya maji , umeme , ufungaji wa mashine za kuchinjia na mifumo ya kupoozea vimekamilika kwa asilimia kubwa.
“Uzalishaji wa kuchinja ng’ombe na mbuzi kuanzia Machi utaajiri wafanyakazi 300 na 120 watakuwa wa kudumu. Tupo katika hatua ya mwisho kila kitu kimeisha, tutakachofanya kuanzia Januari 24, 2022 tutaanza kuleta ng’ombe wa kunenepesha kwa ajili ya kuchinja,” amesema.