Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Machinga walia kuvunjiwa vibanda vyao Iringa

Machinga Pic Machinga walia kuvunjiwa vibanda vyao Iringa

Tue, 6 Jun 2023 Chanzo: Mwananchi

Wafanyabiashara ndogondogo maarufu kwa jina la Machinga wamelalamika kubomolewa vibanda vyao vya biashara katika eneo la Magari Mabovu, Manispaa ya Iringa.

Ubomoaji huo unaodaiwa kufanya na mgambo wa halmashauri huo umefanyika alfajiri, Juni 6, 2022 baada ya kuvamia kwenye eneo hilo kabla Machinga hao hawajafika kwenye maeneo yao ya biashara.

Shughuli ya kuwaondoa wafanyabiashara kando ya barabara ilianza kutekelezwa mwezi uliopita na kusababisha vurugu zilizoifanya Serikali ya Mkoa wa Iringa kusimamia ujenzi wa soko jipya la Mlandege.

Wakizungumza na Mwananchi, baadhi ya wafanyabishara hao walisema ubomoaji huo haujawatendea haki kwani licha ya kuondolewa wameibiwa baadhi ya vitu vyao, huku vingine vikiharibika.

“Tumefika asubuhi na kuona tumebomolewa, hii sio sawa kabisa na huu ni unyanyasaji kwetu. Kwanini waendelee kutufanya hivi? Kwa nini wanafanya tuishi kama wakimbizi ndani ya nchi yetu wenyewe? Hili limetuumiza sana,” amesema Idrisa Kaluma, mmoja wa wafanyabiashara kwenye eneo hilo.

Baadhi ya wanawake hasa mamantilie, waliokuwa wanafanya biashara kwenye eneo hilo wamesema waliacha bidhaa zao jana ikiwemo chakula lakini asubuhi walipofika wamekuta vyakula hivyo vimeharibiwa.

“Maisha yanazidi kuwa magumu, tutawaleaje watoto wetu? Hivi wanataka tuishije sisi? Tunaomba Serikali iangalie suala hili,” amesema Eneo Sanga, mmoja wa Machinga.

Kwa upande wake, Yahaya Mpelembwa amesema ubomoaji huo unatokana na makubaliano waliyofanya ya kuondoka katika maeneo ya barabara.

“Walikuwa wanapaswa kutoka kwenye maeneo ambayo sio ya kufanyia biashara ikiwamo Magari Mabovu, Legeza Mwendo, Miyomboni. Hili ni zoezi la nchi nzima la kuondoa Wamachinga barabarani,” amesema Mpelembwa.

Amesema wamekaa vikao zaidi ya 25 kwa ajili ya kukubaliana na kujipanga kwenye eneo la Mlandege, ambako zaidi ya Sh100 milioni ilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa soko hilo.

“Kule Mlandege wale waliohamia kule walianza kuona kama hakuna kinachoendelea na hiki ndicho kimefanya leo manispaa waje kubomoa eneo hili,” amesema Mpelembwa.

Jitihada za kumpata Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kujibia suala hilo ziligonga mwamba baada ya kufika ofisini kwake na kuambiwa siyo msemaji.

Chanzo: Mwananchi