Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Machinga Manyara, Katavi kupata vitambulisho 56,027

Af8e405f5c73f5cd591a5284ecb9c59c Machinga Manyara, Katavi kupata vitambulisho 56,027

Mon, 19 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Manyara, Joseph Mkirikiti amesema amepokea vitambulisho 56,000 vya wafanyabiashara wadogo maarufu Machinga.

Mkirikiti alisema jana kuwa, atakabidhi vitambulisho hivyo kwa Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Mkoa wa Manyara (TRA) wa mkoa.

Alisema taratibu za sasa ni tofauti na miaka ya nyuma, kwani awali wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri ndio walikuwa wakigawa vitambulisho hivyo lakini sasa utaratibu ni tofauti.

Alisema mameneja wa TRA na watendaji wake katika kila wilaya ndio wahusika wakuu wa kugawa vitambulishi hivyo kwa wajasiriamali hao kwa sababu wao ndio wanaofahamu nani ni mfanyabiashara mdogo na nani mfanyabiashara mkubwa.

Alisema pia ili kudhibiti wasio raia kuchukua vitambulisho hivyo, maofisa wa Idara ya Uhamiaji watahusika katika kuwatambua raia Watanzania wenye sifa ya kupata vitambulisho hivyo.

Mkirikiti alisema katika mikoa ya Manyara, Dodoma, Arusha, Dar es Salaam, Mbeya na ya mipakani watu wengi ambao si Watanzania hujichanganya na kuchukua vitambulisho hivyo.

''Mkoani kwangu tumejipanga, kwa kushirikiana na kwani watendaji wa TRA tutakuwa imara kuhakikisha kila Mmachinga anayestahili kupata kutokana na sifa atapata asiyekuwa na sifa hatapata hata iweje,'' alisema Mkirikiti.

Wakati huohuo, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera alisema amepokea vitambulisho 27 vya Machinga na vyote wamepewa wafanyabishara wadogo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda na Halmashauri ya Nsimbo.

Alisema wanahitaji vitambulisho 24,000 lakini TRA mkoa wa Katavi umewapatia 27 tu.

Homera alisema vitambulisho hivyo vinatengenezwa na TRA mkoa lakini mlolongo wa kuvipata ni mrefu hivyo wana mkakati kuhakikisha vinapatikana na kutolewa kwa wakati kwa walengwa.

"Mimi ukiniuliza majibu yangu ni kwamba mkononi sina kitambulisho chochote, vyote wanavyo TRA, ili kukipata kitambulisho hicho lazima mfanyabiashara mdogo awe na utashi wake mwenyewe aamke na kwenda TRA akapige picha na taratibu nyingine azifuate ambapo atakipata baada ya wiki moja," alisema.

“Inahitajika elimu ya kutosha kwa wananchi ili wafahamu namna ya vitambulisho hivyo vinavyopatikana.Awali ilikuwa rahisi unakutana na wafanyabaishara wadogo mitaani na kuwagawia na wao wanakupatia fedha kila mmoja Sh 20,000 kama dhamana, sasa hivi lazima uende TRA ukajiorodheshe na kupigwa picha na taratibu nyingine kama utakavyoelekezwa.”

“Wafanyabishara wadogo wao wanataka wakilipa fedha yao Sh 20,000 wavipate siku inayofuata,” alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz