Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Mabosi’ wa ombaomba kusakwa

Ombaomba (600 X 303) ‘Mabosi’ wa ombaomba kusakwa

Tue, 4 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imeandaa mkakati wa kuondoa ombaomba mitaani na kuwakamata watu wanaowatumikisha watu wenye ulemavu na watoto kuomba fedha.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum, Amon Mpanju alisema Oktoba mwaka huu wizara hiyo itakaa na watendaji wa Wizara ya Tamisemi, wizara ya Mambo ya Ndani na ya Katiba na Sheria ili kuweka mkakati wa operesheni hiyo.

Mpanju alitoa kauli hiyo wakati wa kongamano la watu wenye ulemavu jijini Mwanza lililolenga kuwajengea uwezo kutumia fursa zilizopo kujikwamua kiuchumi.

“Tutaanza operesheni ya kukamata hao majambazi wanaotumia maskini, watoto, wenye ulemavu kujikusanyia fedha kinyume na utaratibu na tutawashughulikia, haitajalisha nani yuko nyuma ya mtandao huo,” alisema.

Alisema vitendo vya kutumia watoto na watu wenye ulemavu kujipatia fedha ni kinyume na sheria ndogo za manispaa, sheria ya watu wenye ulemavu inayoelekeza kuheshimu utu wa mtu mwenye ulemavu na sheria ya mtoto ya mwaka 2009 inayohimiza kulinda utu wa mtoto.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu (Shivyawata) Wilaya ya Nyamagana, Melkizedeck Mungule aliomba utekelezaji wa operesheni hiyo uharakishwe ili kuyanusuru makundi ya watu yanayotumikishwa.

Mkazi wa Nyakato mkoani Mwanza, Veronica Mtilo alisema utumikishwaji wa makundi maalumu kuomba fedha unatakiwa kupingwa na kila mtu kwa kuwa unadumaza makundi hayo kwa kuwafanya wajione wanapaswa kuwa tegemezi siku zote.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live