Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maboresho Bandari Kigoma yaongeza mizigo, mapato

Bbfbefe6f28ba0cd60538eabe1ed5fca Maboresho Bandari Kigoma yaongeza mizigo, mapato

Sun, 7 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Deusidedit Kakoko amesema maboresho makubwa yaliyofanywa katika Bandari ya Kigoma, yameanza kuleta matokeo chanya ikiwemo kuongezeka kwa shehena ya mizigo na mapato.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika Bandari ya Kigoma, Kakoko alisema shehena na mapato katika bandari hiyo yameongezeka kiasi cha kuipiku Bandari ya Mwanza, ambayo ndiyo iliyokuwa ikiongoza kabla ya maboresho hayo.

Alisema Bandari ya Kigoma inayohusisha bandari zote zilizopo katika Ziwa Tanganyika, ilianza kufanyiwa maboresho kuanzia mwaka 2016/2017 ikihusisha ujenzi wa magati, ununuzi wa mitambo, ujenzi wa maghala, majengo ya abiria na ujenzi wa ofisi za kisasa za makao makuu ya bandari hiyo, ambazo ziko katika hatua za mwisho kukamilika.

Aliongeza kuwa maboresho hayo, yalisukumwa na kasi kubwa ya ongezeko la mahitaji ikilinganishwa na miundombinu iliyokuwepo.

Alisema bandari za Ziwa Tanganyika zimekuwa kiungo kikubwa cha biashara kati ya Tanzania na nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi na Zambia, biashara kubwa ikiwa ni mazao yanayozalishwa Tanzania.

Kutokana na hali hiyo, alisema bandari hizo zimekuwa kichocheo kikubwa cha kukuza uchumi wa wananchi wa mikoa inayozunguka Ziwa Tanganyika, kwani mazao yao yanapata wanunuzi wengi wanaovutiwa na maboresho ya bandari.

Alisema pia bandari hizo pamoja na kuanza kazi kwa reli, kumepunguza bei za bidhaa zinazosababishwa na gharama kubwa za usafirishaji.

Alisema bado kuna maboresho zaidi yanaendelea katika bandari Kuu ya Kigoma, yanayohusisha ujenzi wa gati ya Kibirizi, gati ya abiria na makasha na ujenzi wa bandari kavu ya Katosho.

"Tumekusudia kuifanya bandari ya Kibirizi na Kigoma kuwa ya mizigo ya nje na ile ya Katosho itakuwa ya ndani, " alisema Kakoko.

Alisema matarijio ni kuongezeka zaidi kwa shehena na abiria ni makubwa, kutokana na maboresho ya meli yanayotarajiwa kufanywa na Kampuni ya Huduma za Meli zikiwemo MV Mwongozo, MV Liemba na MT Sangara.

Chanzo: www.habarileo.co.tz