Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mabomu yatumika kutawanya wananchi, wawili washikiliwa

24675 Pic+mabomu TanzaniaWeb

Wed, 31 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbogwe. Polisi wamelazimika kutumia mabomu ya machozi kutawanya kundi la wananchi waliovamia kituo kidogo cha polisi kata ya Lulembela wilayani hapa wakihitaji kukabidhiwa watuhumiwa wawili wanaodaiwa kuiba ng’ombe watano.

Wananchi hao walitaka kuwaua watuhumiwa hao kwa madai kuwa wamechoshwa na tabia yao.

Kamanda wa polisi mkoani Geita, Mponjoli Mwabulambo alithibitisha kukamatwa watuhumiwa hao Oktoba 26 wakidaiwa kuiba ng’ombe hao.

Mwabulambo alisema baada ya polisi kuwatawanya wananchi hao kwa mabomu ya machozi, walikwenda kwenye familia za watuhumiwa wakabomoa nyumba zao na kufanya uharibifu mkubwa wa mali mbalimbali ikiwamo kuua ng’ombe kwa kuwakatakata.

Alisema kwamba mali zilizoharibiwa na wananchi thamani yake haijajulikana na uchunguzi unaendelea.

Naye mwenyekiti wa kijiji cha Lulembela, Juma Galila aliwataja waliokamatwa kwa tuhuma ya wizi kuwa ni Maisha Charles na Martini Simon.

Galila alisema mifugo iliyouawa na wananchi ni ng’ombe 26 na mifugo mingine ikiwamo kuku, kanga, mbwa na paka vyote mali za Charles.

Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Martha Mkupas alisikitishwa na tukio hilo na kutoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi wanapowatilia shaka watu kuhusiana na uhalifu, badala yake watoe taarifa kwenye vyombo vya dola.

Chanzo: mwananchi.co.tz