Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mabehewa 16 yaleta ahueni usafiri Kilimanjaro

A0976625 D9AB 44A4 BAA1 8260ADB09EDF.jpeg Mabehewa 16 yaleta ahueni usafiri Kilimanjaro

Thu, 22 Dec 2022 Chanzo: Mwananchi

Ujio wa mabehewa mapya 16 yanayofanya safari kati ya Dar es salaam na mikoa ya Kaskazini umetajwa kuleta matumaini ya uhakika wa usafiri hususani katika kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi Desemba 22, 2022 na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu wakati wa mapokezi ya treni hiyo yenye mabehewa16 yenye uwezo wa kubeba abiria 1,000 katika stesheni ya reli Moshi mkoani Kilimanjro.

Amesema katika kipindi hiki cha msimu wa sikukuu abiria wamekuwa wakiteseka kutokana na kukosekana kwa usafiri lakini kutokana na uwepo wa treni hawatarajii kupata malalamiko ya wananchi kukosa usafiri au kulanguliwa kwa kutozwa nauli za juu.

"Kipindi kama hiki miaka ya nyuma kulikuwa na changamoto kubwa sana ya usafiri na nauli kuwa juu, kuna watu walikuwa wanatapeliwa kwenye mabasi na kuuziwa tiketi mara mbili mara tatu na nauli zilikuwa zikipandishwa kiholela lakini sasa mwarobaini umepatikana.

"Mheshimiwa Rais ametuletea mwarobaini kwa hiyo wananchi 1000 kupanda treni kwa wakati mmoja sio mchezo na nauli zetu za treni sasahivi ni bei nafuu na kila Mtanzania ataweza kusafiri bila changamoto yoyote," amesema.

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa amewataka abiria kulinda na kutunza mabehewa hayo na miundombinu iliyopo ndani ili yaweze kudumu kwa kizazi cha sasa na baadae.

Akizungumza wakati wa kukabidhi mabehewa hayo, mkurugenzi wa uendeshaji wa TRC, Focus Sahani amesema ujio wa mabehewa hayo 16 ni chachu ya kupunguza adha ya usafiri katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini, katika msimu huu wa sikukuu za mwisho wa mwaka.

"Abiria 1000 ni sawa na mabasi 20, sisi kama reli tunaipenda Kilimanjaro na ndio maana nilipoelekezwa mara moja serikali yetu kuhakikisha tunafufua reli hii na kufanya kazi kwa weledi na kwa usikivu," amesema.

Wakizungumzia ujio wa treni hiyo baadhi ya wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro waliopanda treni hiyo wakitokea Jijini Dar es salaam hadi Moshi, wameishukuru serikali kwa kuwaletea usafiri huo na kwamba itapunguza changamoto ya usafiri kipindi hiki cha msimu wa sikukuu ambapo mkoa huo unakuwa na wageni wengi na kusababisha adha ya usafiri.

Naye Neema Msama, mmoja wa abiria waliosafiri na treni hiyo wameeleza namna walivyosafiri na treni hiyo bila bugdha huku wakisifia huduma bora walizozipata katika usafiri huo pamoja na gharama nafuu. "Tumesafiri vizuri bila changamoto yoyote na huduma zilizokuwa zikitolewa ndani ya treni ni nzuri maana watoa huduma ni wasafi na hakukuwa na changamoto yoyote,"

Chanzo: Mwananchi