Ulikuwa moto kwenye kikao cha Baraza la Madiwani Magu, pale tuhuma za kupotea mali za mradi huo ikigubika mjadala na kugusa madai ya wizi wa vifaa vilivyokuwa vya ujenzi wa kituo cha afya kata ya Shishani wilayani humo.
Ni hoja zinazoelekeza kidole moja kwa moja, kwa mtendaji mwandamizi wa kata Shishani na mlinzi katika kituo kimoja cha afya na mganga.
Ikaelezwa kikaoni, vifaa vilivyobainiwa na kukamatwa katika uchunguzi wa jopo la madiwani, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Mpandalume Simon ni mabati 81 yaliyonunuliwa na serikali kila moja shilingi 55,000 yalikutwa yameezekewa nyumba mbalimbali za watu binafsi katika kata hiyo.
Mwenyekiti Simon akakiambia kikao hicho kwamba, baada ya kuyakamata mabati hayo kwenye nyumba hizo, wamiliki wa nyumba hizo binafsi walihojiwa na kukiri kuuziwa na watumishi hao.
‘’Baada ya kuyakamata mabati hayo yakiwa yameezekewa nyumba za watu binafsi katani hapo, wenye nyumba walikiri kuuziwa na watumishi hawa akiwemo mlinzi wa kituo hicho kwa bei ya shilingi 35,000 kila bati moja ambalo serikali imenunua shilingi 55,000 kila moja,” anasema Mwenyekiti Simon.
Vifaa vingine vilivyokamatwa ni vigae maboksi matano vilivyokuwa vimefichwa shambani kwa kuchimbiwa chini, pia vifaa vya ujenzi ‘ jipusam’.
Mwenyekiti Simon anabainisha kuwa, katika kudadisi wizi huo, mlinzi wa kituo cha afya akakiri kushirikiana na watumishi hao kuzitoa kwa awamu, baada ya kuahidiwa kupewa fedha, lakini baadaye walimpa fedha kidogo tofauti na makubaliano yao, hivyo na yeye akaamua kuiba mabati matano akayauza.
Pia,akafafanulia kikao akimnukuu mlinzi kwamba aliamua kutoboa siri nzima ya wizi alipobanwa, huku watuhumiwa wengine wamekataa kukiri kuhusika, wakimuelekezea dai mlinzi.
Baraza la Madiwani wilayani humo likalalamika, pia kushangazwa na kitendo kilichofanywa na watumishi wa serikali, wakamuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Fedelica Myovella, awachukulie hatua za kisheria watuhumiwa, ikiwamo kuwasimamisha kazi kupisha uchunguzi.
Ni suala lililoungwa mkono na madiwani wote waliomtaka Mkurugenzi Mtendaji kutekeleza maagizo yao ya kuwasimamisha kazi watumishi wanaotuhumiwa kujihusisha na wizi.
Makamu Mwenyekiti pia wa halmashauri hiyo, Faustine Makingi, anaungana na ombi la kuwachukulia hatua, ikianzia na kuwasimamisha kazi wahusika wanaotuhumiwa na kashfa hiyo.
‘‘Tunakuagiza baraza hili, Mkurugenzi kuwachukulia hatua watumishi hawa waliohusika na wizi wa vifaa vya ujenzi wa kituo hicho cha afya kata ya Shishani, ikiwamo kuwasimamisha kazi kupisha uchunguzi zaidi uendelee,” anatamka Mwenyekiti Simon.
Katika kikao hicho cha bajeti ya robo ya pili ya mwaka wa fedha 2023/24, Mwenyekiti akaeleza kushangazwa na wahusika wanaokabiliwa na tuhuma za wizi, kuendelea kuonekana kazini pasipo Mkurugenzi Mtendaji kuchukua hatua stahiki za kiutumishi.
Vilevile, Mwenyekiti Simon akaeleza kukerwa na kitendo cha kuwasilishwa taarifa za miradi ya maendeleo ya kata hiyo, pasipo kuingizwa taarifa za wizi wa vifaa hivyo, akidai “kuna siri nyuma ya pazia ikiendelea.”
BAJETI ILIVYO Katika halmashauri hiyo bajeti ya mwaka wa fedha 2023/24, imepitisha kiasi cha shilingi bilioni 4.8, baada ya kuona uwezo wake umeongezeka, huku Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali ya Mitaa (TAMISEMI) ikiwaongezea shilingi milioni 100, hata bajeti hiyo kufikia shilingi bilioni 4.9 kutekeleza miradi ya maendeleo wilayani humo.
Kuhusu fungu la fedha zinazotolewa na halmashauri kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu kupitia vikundi, Mwenyekiti Simon anaeleza kuwa zipo shilingi milioni 300 katika akaunti ya halmashauri hiyo.
Anasema fedha hizo zimesitishwa kutolewa kutokana na udanganyifu wa watendaji na viongozi wa serikali, kwamba wanasajili vikundi baadhi vikiwa ‘hewa’ na majina yake hayaeleweki.
Simon anazitaka kamati za maendeleo ya kata, kusaidia kusimamia vikundi hivyo ili kujiridhisha na uhalali wa vikundi hivyo, kabla ya kupatiwa walichoomba.
Mwenyekiti anasisitiza haja ya kutolewa elimu katika mikutano ya hadhara, ikiwamo ya kisiasa.Anasema watendaji wa serikali wana wajibu wa kuhakikisha wanaielimisha jamii kufahamu yote yanayofanywa na serikali, kuanzia ngazi ya juu na namna inavyowanufaisha, wilayani Magu.
KAULI YA DED Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Fedelica Myovella, anakiri kuwapo tukio la wizi na anapokea agizo la Mwenyekiti wa Halmashauri na Baraza la Madiwani kuwasimamisha kazi watumishi wanaoshukiwa, ili wapishe uchunguzi.
“Watendaji na watumishi wa serikali wasimamie vema miradi ya maendeleo, fedha zilizopelekwa katika miradi ya maendeleo kutoka mapato ya ndani ni asilimia 65, maelekezo ya serikali ni asilimia 40 kupeleka serikalini,” anasisitiza Myovella.
Myovella anawataka watendaji wa vijiji na kata kutoa taarifa za mapato na matuimizi ya miradi ya maendeleo ya wananchi inayotekelezwa, kila baada ya miezi mitatu, ili kuondoa udanganyifu unaojitokeza.