Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mabasi yawalaza abiria 120 kituo cha polisi

10665 Pic+mabasi TanzaniaWeb

Thu, 5 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Geita. Ili kukabiliana na ajali za barabarani, polisi mkoani Geita linawashikilia madereva wawili wa kampuni ya mabasi ya King Msukuma kwa makosa ya kuendesha magari yakiwa mabovu na kuhatarisha usalama wa abiria.

Mabasi hayo, moja lilikuwa likitoka Mwanza kwenda Kagera na jingine likitokea Kagera kwenda Mwanza. Umbali wa kutoka Mwanza hadi Kagera ni kilomita 406, kwa mwendo wa kutembelea kilomita 80 kwa saa, gari linatakiwa kutumia saa tano au sita.

Ubovu wa magari hayo ulisababisha abiria 120 kulazimika kulala kwenye Kituo Kikuu cha Polisi Geita hadi walipoletewa usafiri mwingine juzi asubuhi na kuendelea na safari zao.

Kamanda wa polisi mkoani Geita, Mponjoli Mwabulambo alisema jana kuwa magari hayo yalikamatwa juzi saa 11:00 jioni katika operesheni ya ukaguzi inayoendelea mkoani hapa.

Mponjoli alisema katika operesheni walikagua magari 59 kati ya hayo, 47 yalikutwa na makosa madogomadogo na kutozwa faini, mawili yalikuwa na matatizo makubwa na kuzuiwa kuondoka huku mengine yakiruhusiwa kuendelea na safari baada ya kuonekana hayana tatizo.

Naye ofisa usafirishaji Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) mkoani hapa, Emily Hagai alisema operesheni hiyo ni endelevu na kuwataka wamiliki na madereva kutii sheria na taratibu zilizopo.

Hagai alisema kukamatwa kwa magari ya King Msukuma kumetokana na taarifa za abiria waliolalamika kuharibika mara kwa mara wakiwa safarini na kuhofia maisha yao.

Baadhi ya abiria waliokuwa katika magari hayo walilalamika kucheleweshwa katika safari zao na kulazimika kulala polisi, huku wakiwa na watoto wadogo na wengine wagonjwa.

Mkazi wa Bukoba, Pablis Paulo alishauri polisi kukagua magari kabla ya kuanza safari ili kuwaondolea abiria usumbufu wa kulala njiani.

Ukaguzi wa magari mkoani Geita ulianza Juni 18 baada ya kutokea ajali ya gari la King Msukuma iliyotokea Juni 17 na kusababisha vifo vya watu watano na majeruhi 36.

Jitihada za polisi

Kutokana na ajali zilizotokea kwa siku 17 na kusababisha vifo vya watu 47 katika mikoa ya Mbeya na Pwani, Mkuu wa Polisi nchini (IGP), Simon Sirro jana alitangaza mabadiliko ya makamanda wa polisi kwa baadhi ya mikoa ili kuimarisha usalama wa abiria.

Juni 14 katika ajali iliyotokea Mbeya, ilisababisha vifo vya watu 13 waliokuwa wakisafiria kutoka Tabora kwenda Kikosi cha Jeshi 844 Itende Mbeya kwa mafunzo ya vitendo.

Ajali nyingine ilitokea Juni 25 wilayani Mkuranga, Pwani na kusababisha vifo vya watu 14 wakiwamo 10 wa familia moja.

Julai mosi, ajali nyingine ilitokea Mbeya na kusababisha vifo vya watu 20 na 45 kujeruhiwa.

Chanzo: mwananchi.co.tz