Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mabasi ya abiria Morogoro yatakiwa kuhamia stendi mpya

Msamvu Morogoro Mabasi ya abiria Morogoro yatakiwa kuhamia stendi mpya

Mon, 28 Aug 2023 Chanzo: Mwananchi

Wamiliki wa mabasi na wasafirishaji abiria wanaokwenda wilaya mbalimbali za Mkoa wa Morogoro wametakiwa kutii agizo la Serikali la kuhamia Stendi ya Mabasi ya Mafiga iliyopo Manispaa ya Morogoro ambayo imejengwa Sh5 bilioni.

Wito huo umetolewa na Diwani wa Kata ya Mafiga, Thomas Butabile baada ya kufika katika stendi hiyo na kukuta idadi ndogo ya mabasi ya wilayani yaliyoitikia agizo hilo huku wamiliki na wasafirishaji wengine wakiendelea na mgomo wa kutopeleka mabasi yao katika stendi hiyo na hivyo kusababisha usumbufu na adha kwa abiria.

Diwani huyo alisema kuwa mpaka sasa utekelezaji wa agizo kwa wamiliki na wasafirishaji umekuwa mdogo hata hivyo wanatakiwa kutambua kuwa jukumu la kusafirisha abiria lipo kwenye mkataba wa leseni zao pia agizo la kuhamia mafiga limetoka kwenye kikao cha Baraza la Badiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.

"Hii Stendi ya Mafiga imejengwa kwa gharama kubwa hatuwezi kukubali kuona inakaa bila kufanya kazi, hawa wasafirishaji wanatakiwa kuelewa hakuna mji wowote unaoweza kuendelea bila kupangwa na stendi hii ni moja ya mipango ya kupanua mji wetu wa Morogoro, hii Stendi ya Mafiga ipo ndani ya Manispaa na wala siyo nje ya Manispaa," amesema Butabile.

Hata hivyo amesema kuwa zipo changamoto ndogondogo katika stendi hiyo ya Mafiga ambazo katika kipindi kifupi zitafanyiwa marekebisho ikiwemo changamoto ya miondombinu ya taa na kwamba kuhusu usalama upo mpango wa kuweka kituo kidogo cha polisi ndani ya stendi hiyo.

Baadhi ya wasafirishaji wa mabasi yanayokwenda wilayani wamesema hawapingi kwenda Mafiga isipokuwa kutokana na stendi hiyo kukaa kinyume kwao inakuwa vigumu kupata abiria.

Mmoja wa wasafirishaji hao Hamis Shabani ameshauri stendi hiyo itumike kwa mabasi yanayotokea njia ya Iringa, huku mabasi mengine yanayotokea njia ya Dodoma yabaki pale pale Stendi ya Msamvu ili kuwaondolea usumbufu abiria hasa wanaotoka mikoa ya mbali ambapo wamekuwa wakifika usiku.

"Awali stendi hii ilipangwa kuwa ya daladala sasa hivi imekuwaje tena kushughulika na watu wa daladala na kuhamia kwetu watu wa mabasi ya wilayani, suala la usafiri kwa Serikali lisiwe biashara bali lione ni huduma muhimu kama huduma nyingine," amesema Shaban.

Mgomo huo licha ya kuathiri wasafiri wanaokwenda wilaya mbalimbali lakini pia umeathiri wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama Machinga pamoja na mama lishe katika Stendi ya Msamvu ambapo amesema kuwa tangu mgomo huo ulipoanza juzi mauzo yao yameshuka.

Ally Amir ni mmoja wa wafanyabiashara ndogondogo katika stendi ya msamvu amesema kuwa suala la mabasi ya wilayani kuhamia Mafiga kutawafanya biashara zao kuyumba kutokana na mzunguko mdogo wa fedha uliopo katika stendi ya Mafiga.

"Wengi wetu humu tumechukua mikopo tunategemea hizi biashara tuweze kurejesha sasa leo ni siku ya tatu hatuuzi kama tulivyozoea tukienda kule Mafiga tunakuta hakuna abiria, kwa kweli tunaomba Serikali isitazame wasafirishaji peke yao watutazame na sisi machinga," amesema Amir.

Naye wakala wa mabasi ya wilayani, Mary Christopher amesema kuwa tangu mgomo huo ulipoanza juzi abiria wanaotoka mikoa ya kusini na hata magharibi wamekuwa wakuteseka na wengine kujikuta wakilala stendi hapo Kwa kukosa nauli ya kwenda mafiga kutafuta mabasi ya kwenda wilayani.

"Leo hii kuna abiria katoka Mwanza anakwenda Ifakara kwenye msiba kafika hapa hakukuwa basi hata moja na nauli ya kwenda mafiga imebidi nitoe hela kumnunulia juisi mtoto wake huku yeye akiendelea kutafuta msaada wa kufika Mafiga," amesema Mary.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia wa simu Meya wa Manispaa ya Morogoro, Pascal Kihanga amesema tayari maamuzi yameshatolewa lililobaki ni utekelezaji.

Chanzo: Mwananchi