SIKU chache baada ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuwatangazia wateule wake kuhakikisha wanashughulikia kero ili viongozi wakuu wa nchi wasikute mabango ya malalamiko, wananchi wa Simiyu wameanza kuibuka na mabango hayo.
Mabango hayo ni mwendelezo wa mgogoro wa mara kwa mara kati ya wachimbaji wadogo na watu wanaopewa leseni za uchimbaji na tume ya madini katika mgodi wa Bulambaka ulioko katika Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu.
Mgogoro huo umewalazimu wachimbaji wadogo kuandamana katika Ofisi ya Mkuu wa wilaya na mkuu wa Mkoa, huku wakiwa wamebeba mabango yenye jumbe za kumkataa mwekezaji aliyepewa leseni ya uchimbaji kwenye mgodi huo.
Wakiongea na waandishi wa habari, wachimbaji hao wakiwemo wamiliki wa mashamba, wamesema wameamua kufanya maandamano ili kupaza sauti zao kwa viongozi wakuu wa taifa.
Wamesema kuwa hatua zilizotumika kupatikana kwa mwekezaji huyo, zimegubikwa na usiri mkubwa, huku wakitaja uwepo wa viashiria vya rushwa katika upatakanaji wake.
“Kwanza hii leseni imetolewa haraka haraka katikati ya kipindi cha maombolezo ya kifo cha aliyekuwa Rais Hayati Dk John Pombe Magufuli, tulijiuliza kwa nini itoke sasa hivi? Na kwa haraka kiasi hicho? Tulipouliza wakasema huu ni utawala mpya siyo ule wa zamani wa Rais Magufuli, huo umepita,” alisema Nyakelenge Gidioni.
Hata hivyo wachimbaji hao wamesema kuwa, wamiliki wa mashamba katika mgodi huo kwa muda wa mwaka mzima, wamekuwa wakihangaikia wapate leseni yao kutoka tume ya madini licha ya kukamilisha taratibu zote za uombaji.
“Tuliambiwa tuunde kikundi ili na sisi tupatiwe leseni ya uchimbaji, leo hii takriban mwaka mzima tumehangaika kupata hiyo leseni lakini tumeshindwa, ila huyu bwana aliyepewa yeye ameomba hivi karibuni na amepata haraka haraka wakati sisi tumehangaika mwaka mzima,” alisema Masuka Sahani, mchimbaji.
Mmoja wa wachimbaji hao Masunzu Mboje alisema kuwa mwekezaji huyo baada ya kufika kwenye mgodi huo, aliwataka wamiliki washamba kusaini hati ya makubaliano kwa nguvu huku wengine akiwapatia pesa (rushwa) ili waweze kusaini.
“Alipokuja alituita wenye mashamba akawa anatoa milioni 10 kwa kila mmoja, mimi nilikataa nikasema siwezi kusaini na kupokea rushwa hiyo mpaka nijue hatma yangu kwenye leseni hii, baadhi yetu walipokea,” alisema Mboje.
Mkuu wa Wilaya, Festo Kiswaga akiongea na wachimbaji hao, alisema kuwa Ofisi yake haitambui leseni hiyo na wala hawezi kuongea jambo lolote juu ya mgogoro huo kwa sababu alitoa maelekezo na yameshindwa kutekelezeka na ofisi ya madini mkoa.
“Mimi najua kila kitu kinachoendelea huko, na hiyo leseni imetoka kinyemela na ofisi yangu haitambui, ila siwezi kusema lolote, niwatake nendeni kwa mkuu wa mkoa, maana ofisi yangu imeshindwa kwani nimetoa maagizo ila wamegoma kutekeleza,” alisema Kiswaga.
Naye mwekezaji huyo Hussen Makubi akiongea na waandishi wa habari juu ya tuhuma hizo, alisema kuwa yeye na wenzake wanaounda kikundi cha Buruwadu 4 Mine ndiyo wamepewa leseni ya kuchimba kwenye mgodi huo.
“Siyo kweli kuwa mimi ndiye nimepewa leseni, ila ni kikundi ambacho wapo hao wenye mashamba, mimi ni mwenyekiti wa kikundi, tupo watu 39 na hizo tuhuma siyo kweli, tulifuata taratibu zote zinazotakiwa,” alisema Makubi.
Hata hivyo, alipotafutwa Ofisa Madini hakuweza kupatikana kwa haraka, kwani alikuwa kwenye kikao cha kamati ya ulinzi na usalama mkoa kilichokuwa kikiendelea katika ofisi ya mkuu wa mkoa kujadili suala hilo.
Kwenye maelekezo yake, Rais Samia alisema endapo yeye au Waziri Mkuu atakuta bango moja katika eneo fulani, mkuu wa wilaya na mkurugenzi watapoteza kazi na vilevile wasiwazuie wananchi kutoa kero hizo na badala yake wahakikishe wanazishughulikia changamoto zote za levo zao kabla ya kiongozi mkubwa kufika.
STORI: MWANDISHI WETU, RISASI