Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mabadiliko yatakayofanywa Coco Beach, "Itafanana na fukwe za Brazil"

077cff02a9dc87036c6eae908d00d69d Mabadiliko yatakayofanywa Coco Beach, "Itafanana na fukwe za Brazil"

Fri, 1 Oct 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, amesema ufukwe wa Coco jijini Dar es Salaam utaendelea kuwa wa umma na utaboreshwa matumizi yake yafanane na fukwe za Brazil na Cuba.

Makalla alisema hayo alipozungumza na watendaji wa wilaya za Ilala na Kinondoni, wadau na wafanyabiashara wadogo kwenye eneo hilo.

Ufukwe wa Coco ni miongoni mwa maeneo maarufu Dar es Salaam ambako wananchi huenda kupumzika, kuburudika kwa vyakula mbalimbali kama vile mihogo, mishikaki, juisi ya miwa na madafu.

"Tuna mpango wa kuboresha Coco Beach, Agha Khan na Kigamboni ili maeneo hayo yatumike vizuri. Tumeandaa mpango wa kufanya eneo liwe na mvuto kwa kushirikiana na wadau wakiwemo kampuni zote za vinywaji, kuwajengea wafanyabiashara mazingira mazuri wauza mihogo na wote waliopo hapo wamepewa kipaumbele hakuna hata mmoja ataachwa,” alisema Makalla.

Alisema ufukwe huo ni eneo pekee la wazi la serikali lililobaki jijini humo baada ya mengine kujengwa. Alisema ni vizuri wananchi walitumie kupumzika na kuburudika.

Makalla alisema kinachofanyika sasa ni kuboresha mazingira ya kufanyia biashara yawe na mvuto, safi, huduma zipatikane ukiwemo muziki, vinywaji na vyakula.

"Tumeshawaratibu wote majina yao wauza mihogo, mishikaki lakini wakiwa na vibanda vizuri vilivyoboreshwa. Tunataka Coco Beach ianze kama kufanana fanana huko baadaye na beach nyingine za Brazil au Cuba ambapo wenzetu wameendelea wanatumia fukwe hizo vizuri," alisema na kusisitiza kuwa usalama kwenye eneo hilo umezingatiwa.

"Hatutaki wahalifu, vibaka nimeshaagiza wakamatwe lakini pia kuwe na watu wa kufanya miamala ya pesa benki ya NMB, CRDB tayari tumeanza kuwa na makubaliano nao, wataweka vibanda vyao hapa vya kutolea huduma," alisema.

Aliwataka wafanyabiashara katika eneo hilo kujiandikisha waweze kuratibiwa vizuri. Hadi jana, walikuwa wafanyabiashara 52 waliojiandikisha.

Mfanyabiashara wa mihogo na mishikaki katika eneo hilo, Constantine Castro, alimshukuru Makalla kwa kuwapa imani kuwa baada ya maboresho wataendelea kuwepo na kupewa kipaumbele kama waanzilishi.

Kiongozi mstaafu wa wafanyabiashara katika eneo hilo, Fatma Machupa, alisema ndoto yao imetimia baada ya kutamani muda mrefu mazingira hayo kuboreshwa.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng'wilabuzu Ludigija, alisema wapo tayari kuifanya kazi hiyo kwa uangalifu mkubwa ili kuhakikisha maeneo ya fukwe yananufaisha wakazi wa Dar es Salaam na mikoa jirani.

Chanzo: www.habarileo.co.tz