Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mabadiliko ya tabianchi yalivyoacha maumivu Jangwani

D0060F4C 6086 4253 85AC FDEF39F7FC13.jpeg Mabadiliko ya tabianchi yalivyoacha maumivu Jangwani

Mon, 19 Dec 2022 Chanzo: Habarileo

Mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha misimu ya mvua kwa mwaka kubadilika, yamekuwa yakirudisha nyuma maendeleo maisha ya mtu mmoja mmoja na kwa taifa kwa ujumla.

Miongoni mwa walioathirika na mabadiliko hayo yapata miaka 11 iliyopita mkoani Dar es Salaam na hata sasa anaishi mkoani humo, ni Sada Msombe. Katika kipindi hicho, aliishi katika Bonde la Magomeni, Mtaa wa Sunna ambaye mabadiliko hayo yamemuachia maumivu makubwa.

Hii ni kutokana na kupoteza majirani zake wawili na vitu vya nyumbani kwa kusombwa na maji yaliyotokana na mafuriko baada ya kunyesha mvua kubwa.

Akielezea tukio hilo, Sada anasema ilikuwa mwaka 2011 katika eneo hilo la bonde walilokuwa wakiishi walipokumbwa na mafuriko yaliyopoteza uhai wa watu na mali zao.

Sada ni mjane ambaye wakati wanakumbwa na mafuriko, mumewe alikuwa amefariki na kumwachia watoto watatu. Watoto wote walinusurika katika tukio hilo baada ya kuokolewa na boti za jeshi.

“Majirani zangu wawili walikufa yaani ukuta wa nyumba ulikatika naona kwa macho yangu, wanachukuliwa na maji naona kwa macho yangu mpaka wanatokomea na natamani nitoke niwasaidie, lakini nashindwa maana sijawahi kuona mafuriko, mbali na kuyaona kwenye TV tu.”

“Tukaokolewa na boti za jeshi tukapelekwa shule ya marehemu Bujugo; alikuwa diwani wakati huo, tukahifadhiwa pale shule zilipokaribia kufunguliwa ndio tukatolewa tukapelekwa Rutihinda, tukaenda Ubungo Maziwa, tukaambiwa tunatafutiwa viwanja, lakini hakuna aliyeamini tungepewa viwanja.”

“Tunamshukuru sana JK (Rais mstaafu Jakaya Kikwete) tukapata viwanja tukiwa kwenye mahema; tukakaa kwenye mahema, siku rais amekuja kututembelea, akakuta yale mahema yana chata ya viroba vyote unavyovijua vya vifungashio vya unga wa ngano au sukari, yaani, viroba unavyovijua; kila mtu kabandika kivyake, akatuahidi kutupatia mifuko 100 ya simenti kila mmoja,” anasema.

Kwa maelezo ya Sada, Rais Jakaya Kikwete kwa kipindi hicho alikuwa madarakani, alitoa msaada huo binafsi si serikali kama asante kwa kutii amri ya serikali ya kuondoka katika bonde lile.

Anasema kaya 604 zilipelekwa Mabwepande, lakini baadaye kaya nyingine ziliwafuata hususani zile ambazo mwanzoni hazikutaka kwenda. Sada anasema kabla ya kununua eneo hilo, aliambiwa mafuriko yaliwahi kutokea mwaka 1978 na ndipo yalipokuja kujirudia tena mwaka huo 2011, lakini baada ya hapo yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika eneo hilo.

Wakati Sada akielezea hayo, Rasi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DUCE), Profesa Stephen Maluka, anasema mabadiliko ya tabianchi ni suala mtambuka linahusu watu wa nchi zote na katika sekta zote.

“Zamani tulikuwa tunasikia mabadiliko ya tabianchi kama ni jambo la kufikirika, lakini sasa hata mwananchi wa kawaida anaelewa. Wote ni mashahidi sasa hivi kila kona Tanzania kilio ni maji, umeme. Kilio ni kila sehemu.” “Mwaka huu Dar es Salaam tumeshuhudia baridi kali. Baridi ipo, lakini mvua hakuna. Mabadiliko ya tabianchi si nadharia, ni hali halisi tunayohitaji kukabiliana nayo,” anasema.

Kwa maelezo yake, zipo athari zinazoonekana moja kwa moja ikiwa ni pamoja na ukame. “Mwaka huu utashangaa kuna ukame, lakini mwaka ujao mvua ikanyesha kukawa na mafuriko. Changamoto hizi zisipochukuliwa hatua za kutosha, huleta madhara makubwa kwa jamii.” Anakwenda mbali na kusema: “Duce kama taasisi ya elimu ya juu inayojihusisha na utafiti, haikuwa nyuma katika kufanya utafiti unaolenga kukabiliana na changamoto zinazotokana na mabadiliko hayo ya tabianchi.”

Anasema hadi sasa chuo kimekuwa kikifanya utafiti juu ya urejeshaji wa matumbawe na mikoko kwa kushirikiana na jamii ya wavuvi kutoka Kata ya Somanga mkoani Lindi. Mhadhiri na Mtafiti Chuo Kikuu Duce, Dk Emiliana Mwita, anasema mabadiliko ya tabianchi yamebadili utaratibu uliozoeleka wa misimu ya vuli na masika kwani sasa mvua na vipindi vya joto hiviendi katika utaratibu uliokuwepo na uliozoeleka.

“Zamani labda kuanzia mwezi Oktoba mpaka Desemba ilikuwa ni vuli kwa Dar es Salaam, sasa hivi hiyo hali haipo tena. Tunaweza kupata mvua zikasababisha mafuriko na mahangaiko kwa maisha ya watu. “Pia kuna vipindi vya joto limepitiliza watu wanahangaika au baridi ambayo imepita kiasi kama baridi tuliyoipitia Dar es Salaam miezi iliyopita,” anasema.

Hata hivyo, Ofisa Mazingira wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam, Fina Bernad, anazungumzia fursa zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi kwa baadhi ya watu kwa kuwa mvua inaponyesha, husomba takataka hadi baharini na huko baharini, kuna watu wanajiajiri kusafisha uchafu huo.

Changamoto iliyopo katika eneo hilo la Temeke anasema ni kutofanyika kwa shughuli za kilimo zilizokuwa zikifanyika. Kwa upande wake Ofisa Mazingira kutoka Jiji la Dar es Salaam, Neema Sita, anasema mabadiliko ya tabianchi yamefanya kuwepo kwa changamoto ya kuongezeka kwa kina cha bahari hali inayosababisha mmomonyoko wa udongo.

Anatolea mfano wa eneo lililopo karibu na Hospitali ya Agha Khan ambako serikali ilijenga ukuta kuzuia maji yasivuke barabara.

“Pia mabadiliko hayo yamefanya maji ya visima yawe na chumvi nyingi. Lakini mikoko inatoweka kwa kukauka. Vilevile Dar es Salaam tulikuwa tunapata mvua mara mbili mwezi Oktoba hadi Desemba na Machi hadi Juni, lakini sasa hakuna mvua kutokana na misimu kubadilika,” anasema.

Akizungumzia mabadiliko hayo, Ofisa Mwandamizi wa shirika lisilo la kiserikali la Global Peace Foundation, Dk Fatma Waziri anasema athari za mabadiliko ya tabianchi ni mtambuka na kama shirika, linaangalia kama mojawapo ya chanzo cha machafuko katika dunia.

“Kunapokuwa kumeharibika katika masuala ya maabadiliko ya tabianchi, hali hiyo inaleta utata unaoweza hata kusababisha mataifa kuingia kwenye mgogoro…” anasema Dk Waziri.

“Kwa mfano, kwa sasa kuna mgogoro ya masuala ya Mto Nile, nchi zinaweza kuingia kwenye machafuko kama hakutaweza kuwa na mazungumzo mazuri ya namna gani ya kufanya utatuzi wa athari za mabadiliko hayo,” anasema.

Kwa maelezo yake hata Tanzania madhara ya mabadiliko ya tabianchi yanaonekana dhahiri kwa kuwa maji yanapokosekana ndani amani inakuwa haipo, hata yanapokosekana katika nchi kunakuwa na shida katika masuala ya amani kwa sababu watu watakuwa na hofu; hawawezi kufanya shughuli zao za kila siku kujiletea maendeleo.”

Anashauri serikali iangalie jambo hilo kama linahitaji kupata sera maalumu inayohusu mabadiliko ya tabianchi. “Sera inayohusika na mabadiliko ya tabianchi bado haijatekelezwa, ipo ndani ya mazingira; kitu ambacho kama wadau tungetamani kuona serikali ikiliangalia jambo hilo kwa upana zaidi,” anasema.

Chanzo: Habarileo