Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mababu kuondokewa kero ya maji

3f82073a84a0c89b5d2dc03d761cd6c5 Mababu kuondokewa kero ya maji

Thu, 4 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAKAZI katika Kijiji cha Mababu kata ya Mababu wilayani Kyela mkoani Mbeya wamebakiwa na siku chache za kusahau kero ya ukosefu wa maji safi na salama iliyowatesa kwa miaka mingi.

Hali hiyo imesababsihwa na awamu ya kwanza ya mradi uliotekelezwa kwa zaidi ya Sh milioni 344 zilizotolewa na serikali kukamilika.

Kwa mujibu wa Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini(Ruwasa) wilayani Kyela, Tanu Deule kinachosubiriwa kwa sasa ni Sh milioni 200 zinazotarajiwa kutolewa na serikali kwa awamu ya pili kukamilisha kazi zilizosalia.

Deule alibainisha hayo wakati Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila alipotembelea mradi huo kwa lengo la kujiridhisha namna fedha zinazotolewa na serikali kwenye miradi ya maji zinavyotumika kuleta unafuu wa maisha kwa wananchi.

Meneja huyo alimhakikishia mkuu wa mkoa huyo kuwa tayari shughuli zote zilizopangwa kufanyika kwenye utekelezaji wa mradi wa Mababu kwa awamu ya kwanza zimekamilika na kinachosubiriwa sasa ni muda wa siku 90 wa uangalizi wa ubora na uwezo wa tangi kuhifadhi maji.

Akizungumzia kero ya maji katika kijiji hicho, Diwani wa kata ya Mababu, Rashid Yahaya alisema wakazi wamekuwa wakilazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo kwenye mito na visima lakini akasema ni jambo la kuishukuru serikali kwa kuwapelekea mradi huo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Klaudia Kita alisema kwa wakazi wa Kijiji cha Mababu kuhakikishiwa kufikishiwa maji ni kama ndoto kwao kutokana na kuteseka kwa muda mrefu, lakini akapongeza jitihada zinazofanywa na uongozi wa juu wa serikali katika miradi akisema kunachochea utekelezaji kwa wakati wa miradi.

Mbunge wa Kyela, Ally Mlagila aliwataka wananchi wilayani hapa kujitoa pale wanapohitajika hususani kwenye kazi za kuchimba mitaro badala ya kusubiri mpaka walipwe, hatua aliyosema inaweza ikawa inachelewesha utekelezaji wa miradi kwenye maeneo yao.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa, Chalamila aliagiza ulinzi kwenye tangi la maji kuimarishwa kwa kujengwa uzio sambamba na wakazi wa maeneo jirani kutambua umuhimu wa mradi huo na kuilinda miundombinu yake.

Chanzo: www.habarileo.co.tz