Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maambukizi ya VVU yaelezwa kuwa tatizo kwa watoto

64086 Pic+vvu

Mon, 24 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Watoto wa kike, wametajwa kuwa wahanga wakubwa wa maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi, kutokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili katika  jamii na kuwafanya kuingia kwenye vishawishi.

Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki, latika lango la Mweka Wilaya ya Moshi na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel, wakati akizungumza kwenye hafla ya kuwapokea wapanda mlima Kilimanjaro 64, waliopanda kwa lengo la kuchangisha fedha za mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Ukimwi, Kampeni ambayo imeandaliwa na Mgodi wa Madini ya Dhahabu Geita, (GGM)

Gabriel alisema katika harakati za mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi, mtoto wa kike ameonekana kuwa mhanga mkubwa wa tatizo hilo hivyo kunahitajika jitihada za makusudi katika kumlinda na kuhakikisha anakuwa salama.

“Kuna changamoto mpya katika mapambano dhidi ya virusi vya ukimwi, kwani  mtoto wa kike ndiye ameonekana kuwa mhanga mkubwa wa maambukizi mapya yanayojitokeza kwenye harakati hizi, sasa tunapaswa kumlinda mtoto wa kike kimkakati,” alisema Gabriel.

Naye Makamu wa Rais wa GGM, Simon Shayo alisema wamekuwa wakifanya kampeni hiyo kwa lengo la kuikumbusha nchi na dunia kuwa Ukimwi ni changamoto ya kiafya na kimaendeleo, ambayo inahitaji juhudi za kila mmoja ili kuweza kuikabili.

 “Tumeanzisha kampeni hii miaka 17 iliyopita, lengo letu likiwa ni kuhakikisha kunakuwa na nguvu ya pamoja katika mapambano dhidi ya Ukimwi, kwani huwezi kuacha zoezi hili kwa serikali pekee, lakini pia tumekuwa tukichangisha fedha kuunga mkono jitihada za serikali na kwa miaka  hii 17, tumechangisha Sh13 bilioni,” alisema Shayo.

Pia Soma

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa  Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), Jumanne Isango alisema kunahitajika ubunifu ili kuongeza hamasa zaidi katika kuupanda Mlima Kilimanjaro kwa ajili ya kuchangisha Fedha za Mapambano dhidi ya Ukimwi.

Isango alisema kampeni hiyo pia imesaidia baadhi ya vikundi vya akina mama wanaoishi na VVU kupewa mafunzo ya ujasiriamali.

Alivitaja vituo hivyo ni Michungwani Handeni- Tanga, Manyoni Singida,  Geita – Geita na Dumila- Kilosa Morogoro ambako ujenzi wake unaendelea.

Isango alisema vituo hivyo vitasaidia kuongeza kasi ya upimaji, upatikanaji wa matumizi sahihi ya dawa ni muhimu katika kufikia malengo ya kufikia 90 -90-90 ifikapo mwaka 2020.

Chanzo: mwananchi.co.tz