Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maajabu shule iliyoshika mkia kiwilaya darasa la saba

80938 Shule+pic

Sun, 20 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Kilomita 90 kutoka katika jiji la Dodoma ndiko iliko Shule ya Msingi ya Chidete iliyopo katika kata ya Makanda Wilaya ya Bahi.

Eneo la Chidete ni kama kisiwa nyakati za mvua kwa kuwa maji hujaa na hivyo kuwa vigumu kwa mtu kuingia au kutoka kitongoji hicho kama hana usafiri unaohimili barabara mbovu zinazojaa maji.

Pia kitongoji hicho kinazungukwa na mto na mbuga za mashamba, hivyo wanafunzi na walimu huishi nje ya kitongoji.

Kuna majengo mawili yenye vyumba vinne na pembeni kuna mtaro unaoonyesha kuwa ni maandalizi ya ujenzi wa jengo jingine kukidhi mahitaji ya madarasa.

Jengo moja hutumika kama ofisi na stoo na kuna nyumba moja ya walimu ambayo ina vyumba vitatu.

Sababu hizo zimetufanya tuitembelee shule hiyo na kujionea mazingira yake, na pengine inaweza kuwa kiwakilishi cha shule nyingine zilizofanya vibaya.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Shule ya Chidete imeshika nafasi ya mwisho katika Wilaya ya Bahi katika matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi.

Uhaba wa vyumba vya madarasa, upungufu wa walimu, umbali wa shule kutoka makazi ya wananchi, mwamko duni wa elimu, miundombinu mibovu na ukosefu wa nyumba za walimu ni matatizo yanayochangia utoaji duni wa elimu na hivyo matokeo mabaya kwa miaka miwili mfululizo, anasema mwalimu mkuu wa shule hiyo, Daniel Msungu.

“Nilipofika mwaka jana shule ilikuwa na walimu wawili ambao walikuwa wanalazimika kufundisha kuanzia chekechekea hadi darasa la saba,” anasema Msungu.

Anasema wanatumia vyumba vitatu kufundishia kwa mtindo wa kuwachanganya wanafunzi wa madarasa yanayokaribiana.

“Chumba kimoja kutumika kwa ajili ya darasa la sita na saba,” anasema Msungu.

“Darasa la tano na nne wanasoma chumba kimoja na darasa la kwanza na la pili chumba kimoja huku darasa la kwanza wakiingia mchana au kusoma chini ya mti. Jumla wanafunzi wangu walikuwa 275.

“Suala la kuchanganya madarasa halikwepeki maana hakuna namna. Hata ukisema waje kwa zamu huwezi. Mtoto akianzia shughuli za nyumbani halafu aje mchana kwa huku unakuwa umempoteza.”

Anasema kabla ya kuongezwa kwa walimu kutoka watatu hadi sita waliona kuwa haingewezekana kutenga zamu za kuingia wanafunzi kwa sababu walimu wangechoka.

Ili kuwezesha wanafunzi wa madarasa mawili kutumia chumba kimoja kwa wakati mmoja, wanafunzi hugawanywa katika makundi kulingana na madarasa yao na baadaye mstari huchorwa katikati kuwatenganisha. Hivyo masomo huanza upande mmoja huku wengine wakisubiri.

“Baada ya kumaliza darasa moja, mwalimu huanza kufundisha waliobakia kwa kutumia ubao huohuo mmoja.”

Uhaba wa walimu

Suala la majengo ni moja ya sababu, lakini uchache wa walimu pia unachangia kufanya vibaya kwa shule hiyo ingawa mwaka huu wameongezwa hadi kufikia sita.

“Walimu walipohamia hapa nikaona mimi na familia yangu tuhamie kwenye fremu ambayo niliijenga kwa ajili ya kufungua duka ili tu waweze kubakia katika shule hii,” anasema mwalimu Msungu.

Anasema ingawa shule hiyo ipo kilomita 18 kutoka makao makuu ya Bahi, mwalimu angeweza kuishi na kufundisha katika eneo hilo lakini haiwezekani kutokana na ubovu wa miundombinu.

“Bado naumiza akili kuhusu hawa (walimu) wanaoishi Makanda katika msimu wa mvua kuna siku hawawezi kuja shule,” anasema akimaanisha eneo wanaloishi lililopo kilomita nane kutoka shuleni.

“Lakini kuwalazimisha waishi hapa siwezi maana hakuna hata kibanda cha kuishi au labda wakae madarasani.”

Hutakiwa kuandika madudu

Suala jingine linalosababisha matokeo mabovu ni mwamko wa wazazi katika masuala ya elimu, anasema Msungu.

“Baadhi ya wazazi huwataka wanafunzi waandike madudu katika mitihani yao ya mwisho ili kukwepa kuwagharamia endapo watakwenda elimu ya sekondari.

Anatoa mfano wa wanafunzi 10 ambao walitarajiwa kufaulu mitihani ya darasa la saba mwaka huu, lakini matokeo yalipotoka ni wanafunzi saba tu ndio waliofanya vizuri.

Anasema pia utoro katika shule hiyo bado ni tatizo kubwa na kwa mwaka huu ni asilimia 45.

Hata hivyo, anasema licha ya mwamko mdogo, suala la umbali pia linachangia matokeo mabaya.

“Kuna wanafunzi ambao hutembea umbali wa kilomita 22 kwenda na kurudi shule, jambo ambalo linawafanya wengine kushindwa kuhudhuria masomo wakati wote,” anasema.

Anasema eneo hilo lina wanyama wakali kama fisi ambao wakati mwingine huwazuia wanafunzi njiani.

“Lakini pamoja na yote hayo tunaahidi tutajitahidi kuinua kiwango cha ufaulu. Mwaka jana walifaulu wanafunzi watatu lakini mwaka huu tuna wanafunzi saba,” anasema.

Pia anamwomba mkurugenzi kuwafikiria walimu wa eneo hilo hata kuwapatia usafiri wa baiskeli kuwawezesha kufika maeneo yenye huduma kama maduka na zahanati.

Wahitimu wasiojua kusoma, kuandika

Katika kile kinachoonyesha kuwa walimu hawawezi kumfikia kila mwanafunzi, Mdemi Sambilwa (16) ni miongoni mwa wanafunzi 20 waliomaliza mwaka huu ambao hawajui kusoma wala kuandika. “Si mimi pekee, wapo wenzangu waliomaliza ambao hawajui kuandika wala kusoma,” anasema.

Sambilwa anasema kila wakati walikuwa wakienda shuleni kwa sababu wasipokwenda wazazi wao wangeitwa na kulipishwa faini.

Hata hivyo, anasema mazingira ya shule yalikuwa ni kuchanganywa madarasa na mara kadhaa walimu wawili waliokuwepo wakiitwa kwenye vikao au kwenda mjini siku za mshahara ni kama shule inafungwa.

Alipoulizwa aliwezaje kuvuka mtihani wa darasa la nne, Sambilwa alisema alirudia mara moja na baadaye kuendelea darasa la tano.

Lakini Msungu alisema kuna miaka ambayo Serikali iliruhusu wanafunzi kuendelea na masomo ya darasa la tano bila kuchujwa.

Naye mmoja wa wakazi katika kitongoji cha Chidete ambaye pia alisoma shuleni hapo, Daudi Hamis alisema aliacha masomo akiwa darasa la saba baada ya kuona hakuna anachokipata shuleni.

“Madarasa yalikuwa mawili tu pale shuleni. Walimu pia walikuwa wachache. Mimi sikufanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba kwa sababu niliona hakuna ninachokipata kwani hadi darasa la saba sikuwa najua kusoma wala kuandika,” anasema Hamis ambaye ni baba wa mtoto mmoja.

‘Ongezeko la walimu limesaidia’

Lakini diwani wa kata ya Makanda, Martine Mazengo ana mtazamo chanya kuhusu shule hiyo. “Ongezeko la walimu limesaidia kuinua kiwango cha ufaulu kutoka wanafunzi watatu hadi saba,” anasema Mazengo.

“Walimu sasa hivi wameongezeka na lile tatizo la kukosekana kwa mwalimu wa kike limekwisha baada ya Serikali kuleta mwalimu wa kike shuleni.”

Anasema pia wamepokea fedha kutoka Mamlaka ya Elimu (Tea) ambazo zitatumika kujenga madarasa manne. “Sasa imebakia tatizo la nyumba za walimu. Tuna nyumba moja tu yenye vyumba vitatu ambayo wanaishi walimu watatu. Mwalimu mkuu amejenga nyumba yake kijiji anachoishi,” anasema.

Naye ofisa mtendaji wa kata hiyo, Emanuel Mahana alisema nguvu ya ziada inatakiwa katika kuisaidia Chidete kwa kuwa hali yake bado ni ya chini.

Chanzo: mwananchi.co.tz