Samaki mkubwa wa ajabu aina ya Popoo (Sunfish) mwenye kilo 142 na urefu zaidi ya sentimita 100, amevuliwa na kutupwa dampo la kisasa lililopo Manispaa ya Mtwara Mikindani.
Tukio hilo lilitokea Julai 3 mwaka huu katika manispaa hiyo, ambapo kutokana na samaki huyo kuwa haliwi na ni wa ajabu na alishaanza kutoa harufu ilisababisha kwenda kutupwa kwenye dampo hilo.
Ofisa Uvuvi wa Manispaa hiyo, Karimu Kassim amesema leo wakati akizungumza kuhusiana na tukio hilo kuwa wamechukua uamuzi wa kumtupa kutokana na kuanza kutoa harufu.
Amesema walishafanya mawasiliano na wenzao wa Marine Park na Taasisi ya Utafiti wa Mazao ya Bahari (TAFIRI) kuhusiana na jambo hilo.
Amesema samaki aina hiyo alivuliwa mwaka 2020, lakini hakuwa mkubwa kama huyo wa mwaka huu ambapo na yeye alitupwa.
Samaki huyo alivuliwa na wavuvi wa hiyari, ambao hutega nyavu zao baharini, ambazo hubeba chochote kilichopo Baharini.
Mvuvi Salmin Halidad amesema kwa muda mrefu anafanya kazi hiyo, lakini hajawahi kuona samaki mkubwa kama huyo.