Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maajabu! Aishi na risasi tatu mwilini kwa miaka 11

Aishi Na Risasi Miaka 11 Maajabu! Aishi na risasi tatu mwilini kwa miaka 11

Wed, 2 Nov 2022 Chanzo: Mwananchi

Julai 6 mwaka 2011 ni siku ambayo hatoisahaulika kwa Kulwa Makasi (32) baada ya kupigwa risasi tatu, moja kichwani, mgongoni na kwenye paja la kulia anazoishi nazo kwa miaka 11 sasa.

Mkazi huyo wa Shibula jijini Mwanza kwa sasa anatembea kwa kiti maalum kutokana na ulemavu alioupata baada ya kupigwa risasi na askari polisi wakati wa operesheni ya kuwaondoa wamachinga katikati ya mji mwaka huo. Kwa ulemavu alionao, familia yake sasa inatunzwa na mkewe, Salome Peter.

Siku ya tukio, polisi kwa kushirikiana na mgambo walikuwa wanawaondoa wamachinga katika Mtaa wa Makoroboi na Kulwa anasema alitoka nyumbani kwake Mtaa wa Mabatini kwenda kwenye biashara zake ndipo alikuta watu wakikimbizana.

“Nilipofika Makoroboi nilikuta taharuki ya Jeshi la Polisi, mgambo na wamachinga. Nikauliza kuna nini, wakaniambia wamesema tusifanye biashara eneo hili, nikasikia sauti ya askari akisema wenye mizigo eneo hili waje waitoe,” anakumbuka Makasi.

Baada ya kusikia kauli ya askari huyo, akiwa na wenzake watatu, anasema waliingia stoo na ndani ya dakika tatu walisikia mabomu ya machozi yakipigwa nje.

“Tulitaharuki, tukaamua kutoka na tukaona watu wanakimbia, nasi tukakimbia kuelekea lilipokuwa Soko Kuu la Mwanza. Tukiwa tunakimbia tulisikia askari akitoa amri kwamba ‘piga risasi.’ Zikanipiga tatu,” anasema.

Kutokana na kutokwa damu nyingi, anasema alipoteza fahamu na alipozinduka alijikuta katika Chumba cha Uangalizi Maalum (ICU) cha Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando alikokaa kwa mwezi mzima lakini hakufanyiwa upasuaji wa kuondoa risasi hizo kutokana na ubovu wa mashine hivyo akapewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambako alikaa kwa mwaka mmoja bila kufanyiwa upasuaji, sababu ikiwa ni hitilafu za mashine.

“Vipimo vya Muhimbili walisema matibabu yangu kwa wakati huo hayakuwepo nchini hivyo nilihitajika kusafirishwa kwenda India kufanyiwa upasuaji huo,” anasema Makasi.

Matumaini yaligonga mwamba baada ya familia yake kushindwa kumudu gharama za usafiri na matibabu ambazo hazikumbuki kutokana na kupoteza karatasi yenye taarifa hizo.

“Baada ya kukaa muda mrefu hospitalini bila matibabu madaktari walishauri nirudishwe nyumbani,” anasema.

Kutokana na risasi zilizo mwilini mwake, Makasi anasema kuna wakati humsababishia hasira jambo linalomfanya aonekane mwenye tabia tofauti kwenye familia na kipindi cha baridi anahisi maumivu na vichomi jambo linalomkosesha usingizi.

Huku akibubujikwa machozi, Salome, mke wa Makasi anasema hakutarajia mume wake angekuwa mlemavu.

“Wakati mwingine nakata tamaa kwa sababu mambo yameniwia magumu mno, nawaomba mtusaidie. Naamini akiondolewa risasi mwilini anaweza kurejea kwenye utimamu wa afya ili tusaidiane kulea hii familia,” anasema.

Kauli ya Muhimbili, MOI

Alipoulizwa kutaka kufahamu kama Makasi alipokelewa, Msemaji wa MNH, Aminiel Aligaesha alisema taarifa za mgonjwa huyo hazionekani.

“Nimeangalia kwenye mfumo sijaona kama alitibiwa hapa Muhimbili, nadhani alipofikishwa hapa alielekezwa kwenda MOI,” alisema Aligaesha

Ofisa Uhusiano wa MOI, Patrick Mvungi naye alisema taarifa za mgonjwa huyo hazioni ingawa suala hilo halizuii mgonjwa kutibiwa.

Chanzo: Mwananchi