Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maafa ya raia, sungusungu mali zikiteketezwa kijijini

CB607AE3 2D15 47F5 BC42 D1460CEF15DD.jpeg Maafa ya raia, sungusungu mali zikiteketezwa kijijini

Tue, 20 Dec 2022 Chanzo: Mwananchi

Mtu mmoja amefariki katika Kijiji cha Mwitikila wilayani Bahi kutokana na kipigo alichokipata kwa tuhuma za uchawi na kuacha uharibifu mkubwa wa mali.

Aliyefariki ni Beritha Chalo (59) ambaye alipigwa na vijana waliotajwa kuwa ni walinzi wa sungusungu waliotumwa na viongozi kuwakamata wachawi na vijana wanaotajwa kuvuta bangi.

Bertha alikutwa nyumbani kwake na vijana hao walioanza kumshambulia kwa fimbo wakimtuhumu kuwa miongoni mwa wachawi na kumwacha akiwa na hali mbaya kabla ya kufariki baadaye usiku.

Mbali na kifo cha Bertha, nyumba, duka na gari linalotajwa kuwa la diwani wa Mwitikila, Aloyce Sokozi viliteketezwa huku nyumba ya mwenyekiti wa kijiji nayo ikivunjwa wakati wakimtafuta.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Martin Otieno amethibitisha kutokea kwa vurugu na mauaji katika kijiji hicho na kwamba jeshi linafuatilia kujua chanzo cha vurugu hizo.

“Hizo taarifa ni kweli nimeshazipata, nimetuma askari wapo huko kufuatilia ili tujue ukweli na nitatoa taarifa kamili ya tukio hilo,” alisema.

Hali ilivyokuwa Job Nhonya mkazi wa kijiji hicho aliliambia Mwananchi kuwa vurugu zilianza juzi mchana baada ya kikundi cha sungusungu waliotumwa na viongozi kuanza kuwasaka walioitwa wachawi na wazururaji.

Nkhonya alisema hali haikuwa nzuri kijijini hapo kwani kila mtu aliyeonekana alikuwa anachapwa fimbo akitajwa kwa lolote.

“Si mara moja au mbili, viongozi huwa wanawaita sungusungu na wanafanya kazi ya kushtukiza kwa kuwavamia watu, wao wanalenga vijana wanaosema ni wazururaji na kuanza kuwapiga. Jana (juzi) mambo yalikuwa magumu sana, watu wazima walikuwa wanakimbia maana wanaweza kukuvamia kwamba una uchawi wakati ulikuwa na kisa na mmoja wa hao sungusungu,” alisema Khonya.

Kwa upande wake, Athony Mshegamo alisema alisikia kelele wakati moto ukiunguza mali za diwani lakini kwa sababu ya ulemavu wake wa mguu hakuweza kutoka nje.

Alisema usiku kulikuwa na vishindo vilivyotokana na milipuko ya mitungi ya gesi iliyokuwa kwenye duka la diwani baada ya moto kuwaka hali iliyowafanya waingiwe na hofu.

Mbunge wa Bahi, Kenneth Nollo jana asubuhi alienda katika kijiji hicho kujionea hali ilivyo na kutoa pole, alisema kumekuwa na ongezeko la vurugu kijijini hapo siku za hivi karibuni.

Akizungumza kwa simu ya mkononi alisema yaliyotokea ni mambo ya hovyo ambayo yameacha hasara kubwa na hofu kwa wananchi hasa kipindi hiki wanapojiandaa na msimu mwingine wa kilimo.

“Nimesikitishwa sana na tabia hii, hadi karne hii bado watu wanatajwa kwa uchawi kweli? Jambo hili limeleta picha mbaya na kwa kweli nalaani vitendo hivi na ningeomba sheria ichukue mkondo wake,” alisema Nollo.

Viongozi watokomea Mbali na vijana wengi kukimbia kijiji hapo kutokana na sakata hilo, diwani na mwenyekiti nao hadi jana hawakujulikana waliko na hata simu zao hazikupatikana siku nzima.

Taarifa zinasema baada ya kutokea kwa tukio hilo, viongozi hao walishauriwa waondoke kwani hali haikuwa nzuri na wananchi walikuwa wakiwatuhumu wao kuwa ndiyo chanzo cha matatizo hayo kutokana na kuendekeza tabia ya sungusungu kuwapiga watu kila wanapolinda mitaa ya kijiji.

Kijiji hiki ni miongoni mwa vijiji maarufu katika Wilaya ya Bahi lakini kwa siku za hivi karibuni kimekuwa na matukio mengi yanayotajwa kuisababishia Serikali na wananchi hasara.

Matukio makubwa ya siku za hivi karibuni katika kijiji hicho kilichopo kilomita 48 kutoka jijini Dodoma ni pamoja na wanakijiji kuwafukuza maofisa wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira (Ruwasa) walioenda kutekeleza miradi ya maji.

Chanzo: Mwananchi