Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ma-RC watakiwa kukomesha uvuvi haramu

Fdb040644f7ce50b21d853685f7a5fc7 Ma-RC watakiwa kukomesha uvuvi haramu

Sun, 7 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amewataka wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi watendaji wa halmashauri nchini, kudhibiti uvuvi haramu kwenye maeneo yao.

Amesema vitendo vya uvuvi haramu bado vinaendelea kujitokeza ndani ya Ziwa Victoria.

Alisema hayo jijini hapa kwenye mkutano wa ulinzi na usimamizi shirikishi wa raslimali uvuvi Kanda ya Ziwa, uliohudhuriwa na wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi watendaji na watalaamu wa sekta ya uvuvi.

Ndaki alisema Ziwa Victoria lenye ukubwa wa kilomita za mraba 68,800, linamilikiwa kwa pamoja na Tanzania, Kenya na Uganda. Tanzania inamiliki eneo la kilometa za mraba 35,088 sawa na asilimia 51 likihusisha mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Simiyu na Mara. Kuna wavuvi wadogo wapatao 109,397 na vyombo vya uvuvi 31,773 katika ziwa hilo.

Alisema rasilimali za uvuvi katika ziwa hilo na manufaa yatokanayo na rasilimali hizo, vinatishiwa na uvuvi haramu ambao unafanyika kinyume cha Sheria ya Uvuvi Namba 22 ya mwaka 2003 na Kanuni zake za mwaka 2009 na marekebisho yake ya 2018, 2019 na 2020.

Waziri Ndaki alisema uvuvi huo haramu unaofanyika ni matumizi ya zana haramu za uvuvi zikiwemo nyavu za macho madogo, nyavu za timba na makokoro. Alisema maeneo mengine uvuvi huo umekuwa ukifanywa kwa kutumia sumu.

“Baadhi ya watu wamekuwa wanavua bila leseni, wanavua maenepo yasiyoruhusiwa na ambayo ni mazalia ya samaki na kutumia vyombo vya uvuvi ambavyo havikusajiliwa, na ndio maana tumewaalika kwenye mkutano huu nyie viongozi wa mikoa na serikali za mitaa, tutafute namna ya kupambana na hali hii,” alisema.

Alisema mbali na uvuvi huo haramu, pia kuna uchakataji wa samaki wasioruhusiwa kisheria.

Alisema madhara hao ya uvuvi haramu, yamesababisha kupungua kwa samaki, mapato ya wananchi, maduhuli ya serikali na kuharibika kwa mazalia.

Alisema kuwa serikali imejipanga kutatua changamoto za sekta ya uvuvi kwa kuandaa mkakati mbadala wa kusimamia na kuendeleza raslimali za uvuvi wa 2021/2022 hadi 2025/2026.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Rashid Tamatamah alisema vifo vya sangara wakubwa vilivyotokea ndani ya Ziwa Victoria mwanzoni mwa mwezi Januari mwaka huu katika maneo ya Sota Rorya mkoani Mara, Nyamikoma Busega mkoani Simiyu, Geita na baadhi ya visiwa vya Ukerewe na Kagera, havikusababishwa na sumu kama ilivyokuwa imefahamika.

Alisema watalaamu wa taasisi ya uvuvi kwa kushirikiana na wale wa maabara ya kusimamia ubora wa samaki Mwanza, walikusanya sampuli za samaki waliokufa katika mikoa hiyo na kuziwasilisha katika maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ambako zilipokelewa wizarani Januari 3 mwaka huu.

Aliwata wananchi wote kutokuwa na hofu ya vifo hivyo vya sangara katika ziwa Victoria.

Chanzo: www.habarileo.co.tz