Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MZOZO MSIBANI: Mazishi mke wa Mangi Marealle II yageuka sinema

99904 Pic+mareale+2 MZOZO MSIBANI: Mazishi mke wa Mangi Marealle II yageuka sinema

Thu, 26 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Ilikuwa kama sinema vile wakati wa mazishi ya bibi kizee, Veronica Marealle (105) baada ya mkuu wa mkoa Kilimanjaro, Anna Mghwira kuzuia, lakini ndugu wakaamua kuzika kama walivyopanga.

Agizo la Mghwira lilisomwa saa 8:30 mchana na mkuu wa Polisi wilaya (OCD) ya Moshi, Mrakibu wa Polisi (SP), Joseph Kate wakati waombolezaji wakijiandaa kubeba mwili kuelekea makaburini.

Mazishi hayo yalifanyika nyumbani kwa marehemu kitongoji cha Moori katika kijiji cha Lyamrakana huko Marangu, katika eneo ambalo marehemu aliacha wosia kuwa akifa, azikwe katika eneo hilo.

Katika ujumbe huo, mkuu wa mkoa aliagiza mazishi hayo yasifanyike katika eneo ambalo liliandaliwa, akisema eneo hilo lina mgogoro hivyo kama ni kuzika, basi azikwe eneo lingine lisilo na mgogoro.

Hata hivyo, baada ya ndugu wa familia ya marehemu pamoja na waombolezaji kujadiliana hadi saa 9:15 alasiri, walikubaliana kuzika eneo hilo hilo kwa vile kulikuwa hakuna zuio la mahakama.

Mwanafamilia, Francis Matunda alisema waliamua kuzika kama walivyopanga, kwa vile wanafahamu misingi ya utawala wa sheria kwamba kama ni kuzuia, ilipaswa kuwe na amri ya mahakama.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Sinema hiyo ilianza saa 4:00 asubuhi wakati polisi wakiwa na magari mawili wakiongozwa na SP Kate na mkuu wa kituo cha Polisi (OCS) cha Himo, Rodgers Tindi kufika nyumbani kwa marehemu.

SP Kate na OCS wa Himo wakawaeleza ndugu wa marehemu kuwa busara itumike ili wasizike na wasubiri kesi iliyofunguliwa Baraza la Ardhi na Nyumba Moshi, itakapotolewa uamuzi kesho.

Hata hivyo, ndugu wa marehemu wakiongozwa na mtoto wa marehemu, Acley Marealle waligoma na kuwaambia kama ni busara, basi busara hiyo hiyo itumike ili wazike kwani hakuna zuio.

Baada ya majadiliano ya karibu dakika 30, maofisa hao wa polisi wakanawa mikono na kuruhusu taratibu za mazishi ziendelee na kuacha namba za simu ili kama kukitokea fujo basi waitwe.

Lakini shughuli zote za mazishi zilifanyika kwa amani hadi ibada ilipomalizika na wakati waombolezaji wakitaka kuelekea makaburini ndipo OCD akaja na ujumbe wa RC Mghwira.

Wakati ujumbe huo ukisomwa, tayari Paroko wa Parokia ya Samanga wa Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi, Padri Ephrem Mapendano, alikuwa ameshamaliza taratibu zote za ibada.

Hata hivyo, baada ya ujumbe kusomwa, kuliibuka minong’ono na baada ya majadiliano na polisi, waliruhusu mazishi yaendelee kwa vile hakuna aliyejitokeza kuonyesha eneo lipi hasa lenye mgogoro.

Mgogoro wa eneo la maziko uliibuka Machi 19, 2020 baada ya mfanyabiashara wa Moshi, Frank Marealle ambaye pia ni Mangi wa Wamarangu, kupinga asizikwe hapo akidai ni eneo lake.

Marehemu alikuwa mke wa mwisho wa Mangi David Mlang’a na ni mama mdogo wa mfanyabiashara huyo na ndio pekee alikuwa amebakia miongoni mwa wake sita wa marehemu Mlang’a Marealle.

Mangi David alipokea umangi kutoka kwa mangi mkuu Marealle wa kwanza mwaka 1916 na akafariki mwaka 1962 na Mangi huyo alikuwa na wake sita, na marehemu Veronica ndio alikuwa mke wa sita.

Katika maombi yake namba 76 ya 2020 aliyoyawasilisha mahakamani, Frank anadai kuwa mmiliki halali wa eneo hilo na kwamba aliidhinishwa na kijiji cha Lyamrakana, Marangu Aprili 29, 2015.

“Mama yangu alikuwa wa kwanza kuishi hapo tangu enzi ardhi hiyo ikiwa haijaendelezwa na watoto wake wote nikiwamo mimi tulizaliwa na kukulia katika eneo hilo hadi leo,” ameeleza Marealle.

Frank Marealle alifungua shauri hilo dhidi ya mtoto wa bibi huyo, Acley Mlang’a Marealle, akidai mtoto huyo ana nia ya kumzika mama yake katika eneo hilo ambalo si la marehemu bali ni lake.

Kupitia kwa wakili wake, Modestus Njau, Marealle alieleza maombi hayo ni ya dharura kwa kuwa Veronica aliyefariki Machi 14,2020 anatarajiwa kuzikwa eneo hilo wakati wowote kuanzia Machi 18.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba Moshi, Silas James hakutoa zuio lolote la mazishi hayo, na kutoa samansi za kuita pande zote mbili ili awasikilize hiyo kesho Jumatatu.

Mjibu maombi katika kesi hiyo, Acley ambaye ni mtoto wa marehemu, aliliambia gazeti hili juzi kuwa eneo hilo ambalo Frank Marealle anadai, ni la mama yake na wameishi hapo tangu kwa miaka mingi.

Wosia wa marehemu alioutoa Aprili 4,2015 , unaeleza kuwa marehemu alimrithisha mjukuu wake shamba hilo lenye ukumbwa wa hekari mbili aliloachiwa na marehemu mumewe.

Chanzo: mwananchi.co.tz