Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MTENDAJI WA KIJIJI: Mwanangu amefia tumboni kwa uzembe waliofanya wauguzi

A9680785e7fe48a60e872c2eb0408295.png MTENDAJI WA KIJIJI: Mwanangu amefia tumboni kwa uzembe waliofanya wauguzi

Mon, 9 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

“BAADA ya muda wa matazamio kwa ajili ya kujifungua kupita, Julai 22 mwaka huu, siku ya Alhamisi nilikwenda hospitali ya Itumba ambayo ni hospitali ya Wilaya ya Ileje (Mkoani Songwe), nilikokuwa nahudhuria kliniki kwa ajili ya kujifungua.

“Julai 24, siku ya Jumamosi nikiwa hospitalini hapo uchungu ulinishika na nilipopimwa ikaonyesha mtoto alikuwa anacheza. Lakini mchana hawakunipima ili kuangalia hali yangu na mtoto lakini uchungu uliendelea. Jioni pia sikupimwa ila tulienda chumba cha mionzi kumuona daktari. Tulipofika daktari alinipiga ultrasound lakini akasema mtoto haonekani vizuri.

“Nilirudi chumba cha kujifungua. Baada ya kurudi uchungu uliniuma sana. Lakini baadae nikaambiwa na daktari kuwa mtoto wangu hayupo hai, amekufa. Kiukweli mimi nilikuwa ninasikia uchungu tangu jana yake Ijumaa lakini licha ya kuwaambia wauguzi kwamba ninasikia huku mwezi wa kujifungua na wiki ya matazamio vikiwa vimepita hakuna aliyejali. Mimi ninaamini ndio sababu ya mwanangu kufia tumboni.”

Hayo ni madai ya Enelka Kibona ambaye ni mama wa mtoto mmoja na huyo aliyefia tumboni alimtazamia kuwa mwanae wa pili.

Enelka ambaye pia ni Mtendaji wa kijiji cha Itumba wilaya ya Ileje, analia na wahuduma wa afya waliokuwa zamu siku hiyo akidai kwamba hawakutoa ushirikiano wa kutosha ili kumsaidia kumtoa mtoto aliyefia tumboni.

Anapoulizwa kwa nini anaamini kwamba kuna uzembe uliosababisha kumpoteza mwanae, Enelka anasema: ‘’Nilitundikiwa dripu ya sindano za uchungu, lakini nilipoomba msaada wa kusaidiwa baada ya uchungu kunizidi wauguzi waliniambia kuwa nawasumbua. Wakawa wanaendelea tu na maongezi yao huku wakiwa busy na simu zao.”

Anadai kwamba baada ya kuona hapati msaada licha ya kupiga kelele aliamua kuchukua kitenge chake na kutandika chini ya sakafu kwa kuhofia mtoto kudondoka chini ikiwa ataendelea kuwa juu ya kitanda kutokana na purukushani ya kusukuma mtoto bila msaada wowote.

“Niliendelea kusukuma mtoto huku nikiwa chini mkono niliotundikwa drip ukiwa juu ya kitanda kwa kuwa nilikuwa nahofia kuchomoa ile drip, baada ya kupiga sana kelele muuguzi mmoja alikuja kuchungulia dirishani ndipo alipomwita mwenzake na kuanza kujiandaa kunisaidia lakini pamoja na maumivu yote hayo mhudumu mmoja aliendelea kunifokea akiniuliza kwa nini nimeshuka kitandani na kusababisha kuchafua sakafu na mashuka kwa damu. Wakati mimi ninahangaika akawa anasema nitalazimika kufanya usafi mwenyewe.”

Anadai alimsikia daktari akiwagombeza wauguzi kwamba kwa kuchelewa kumzalisha kwani Jumamosi asubuhi ambapo uchungu ulimuanza mtoto alikuwa vizuri lakini mchana hawakumpima mpaka ilipofika jioni saa 12 ndipo walipompeleka kwenye ultrasound na kuonekana mtoto alishafia tumboni.

“Yaani ni kwamba muda wote ambao mimi nilikuwa ninasikia uchungu na kutaka kusukuma mtoto, wauguzi walikuwa wanadai kuwa njia haijafunguka na kuendelea kuchati na simu zao (bila hata kujishughulisha kuangalia njia),” analalamika mwanamke huyo.

Enelka anasema mwanae wa kwanza alijifungulia katika zahanati ya Kalembo wilayani humo miaka mitano iliyopita ambako anajuta kwa nini hakurudi huko kwani alihudumiwa vizuri.

Anazidi kudai kwamba aliamini kwenye hospitali ya wilaya angehudumiwa vizuri zaidi kulinganisha na zahanati, hasa kama atapata tatizo la uzazi pingamizi, lakini imekuwa kinyume chake.

Mumewe, Winfrod Kibona anasema: “Niliumia sana kitendo cha kumpoteza mtoto ambaye alikuwa mzima kwa kipindi chote kwa sababu alikuwa anacheza vizuri tumboni.”

MGANGA MKUU WA HOSPITALI YA WILAYA

Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo ya Wilaya, Janeth Makoye, anakiri kupata malalamiko ya mwananchi huyo na kwamba tayari wameanza uchunguzi ili kubaini kama kuna ukweli kwenye madai yake ili waweze kuchukua hatua stahiki.

“Wauguzi waliokuwepo kazini siku hiyo wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi, hivyo tukishapata majibu ya uchunguzi ndio tutajua chanzo cha mwanamke huyo kupoteza mtoto akiwa tumboni,” anasema Dk Makoye.

Kuhusu baadhi ya akina mama na wagonjwa wengine kulalamikia huduma zinazotolewa hospitalini hapo, Dk Makoye anasema hazijamfikia.

Hata hivyo, anawataka wananchi kutoa ushirikiano kwenye ofisi yake pale wanapokutana na changamoto mbalimbali ambazo huwakwamisha kupata matibabu mazuri ambayo ni haki yao.

MKUU WA WILAYA AVALIA NJUGA

Mkuu wa wilaya ya Ileje, Anna Gidarya anasema amesikitishwa sana na kisa cha mtendaji huyo wa kijiji kama anavyosimulia ndivyo alivyotendewa.

“Inasikitisha sana (kama hii ilitokana na uzembe). Huyu mama ni mtendaji wa kijiji ambaye ni mtumishi mwenzao,” anasema na kuonesha kwamba kama mtendaji wa kijiji anafanyiwa hivyo, basi hali inaweza kuwa mbaya sana kwa mwananchi wa kawaida.

Mkuu huyo wa wilaya anasema uchunguzi wa awali aliofanya unaonesha kwamba mama huyo alifanyiwa manyanyaso makubwa.

“Tumeshamwagiza Mganga Mkuu alete maelezo ya kutosha, lakini na sisi tayari tumeshaunda kamati ya kuchunguza, hii ni jinai hivyo tunashirikisha kamati ya ulinzi na usalama,” anasema Gidarya.

Mkuu huyo wa Wilaya na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo anasema pamoja na serikali kufanya jitihada kubwa ya kuboresha miundombinu ya afya ikiwemo Hospitali ya Wilaya ya Ileje kuboreshwa majengo yake, malalamiko ya wananchi kama ya mtendaji huyo yanafanya majengo mazuri ya hospitali hiyo yasiendane na huduma zinazotolewa.

MBUNGE ATOA RAI

Naibu Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Ileje, Godfrey Kasekenya, akisikiliza kero za wananchi katika kata ya Itumba amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo akishirikiana na Mganga Mkuu wa Hospitali kuacha kupuuza malalamiko yanayotolewa na wananchi kuhusu huduma za afya zisizoridhisha hospitalini hapo.

“Hawa wananchi wasikilizwe na kutatuliwa changamoto wanazozisema kuhusu hospitali. Kwa nini kila siku walalamikie hospitali tu? Taarifa ya mama mjamzito kupoteza mtoto kutokana na uzembe hospititalini inasikitisha sana, ifike kipindi tuwaonye hao watumishi,” anasema Kasekenya.

Kitson Sambo, mzee mwenye miaka zaidi ya 70 akieleza kero yake mbele ya Mbunge huyo anasema pamoja na serikali kusisitiza kuwa wazaee wanatakiwa kutibiwa bure, yeye alipofika hospitalini hapo alichaniwa cheti chake na wafanya kazi wa hospitali hiyo wakidai kwamba anawasumbua, wakimtaka awatafute ndugu zake wamlipie matibabu.

WANANCHI WANAVYOSEMA

Ashura John (sio jina halisi) amedai mbele ya mwandishi wa makala haya kwamba binti yake alipoteza watoto wawili kwa awamu tofauti wakati wa kujifungua hospitalini hapo kutokana na kile anachodai ni uzembe wa wauguzi katika hospitali hiyo ya Itumba.

Anasema binti yake alipopata ujauzito tena, hivi karibuni aliamua kutumia gharama kubwa kumpeleka katika hospitali ya Vwawa ambayo ilikuwa hospitali teule ya Mkoa wa Songwe.

“Namshukuru Mungu Mwanangu safari hii amejifungua kwa upasuaji lakini wote na mtoto wanaendelea vizuri kutokana na huduma bora walizopata ,” anasema Ashura.

Naye Hadija Julius (siyo jina lake halisi) anasema rafiki yake alijifungua mtoto ambaye hakufikisha miezi tisa katika hospitali hiyo lakini baada ya kujifungua mtoto huyo hakuwekwa kwenye chumba maalumu cha joto kwa muda mwafaka.

Hatua hiyo anadai ilisababisha mtoto huyo kupoteza maisha muda mfupi baada ya kuhamishiwa katika hospitali ya Mbalizi mkoani Mbeya.

Anasema walipofika Mbalizi waliambiwa kuwa mtoto alicheleweshwa kuwekewa joto ambalo ni muhimu kwa mtoto anayezaliwa bila kufikisha miezi tisa.

“Kuna baadhi ya akina mama hasa vijijini hivi sasa wanaona ni bora wajifungulie majumbani mwao kuliko kwenda Itumba kutokana na changamoto za kufokewa na kutosaidiwa pindi wanapohitaji msaada wanaposhikwa uchungu,” anadai Hadija.

KAULI YA MGANGA MKUU WA MKOA

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Songwe, Lukombodzo Lulandala ambaye pia ni daktari bingwa wanawake na watoto, anasema kwa kawaida uchungu wa kujifungua ukishaanza ndani ya saa 16 huwa wanategemea mama ajifungue.

Anasema uchungu ukizidi saa hizo matabibu wanalazimika kumfanyia upasuaji mjamzito husika ili kumnusuru mama na mtoto kupoteza maisha.

Kuhusu mama kupitiliza muda wa kujifungua baada ya miezi tisa kutimia ikiwa ni pamoja na siku za matazamio Dk Lulandala anasema: “kwa kawaida mtoto inatakiwa akae tumboni wiki 40 ambazo ni sawa ni miezi tisa, hivyo ikiwa wiki hizo zimeisha maisha ya mtoto tumboni huwa hatarini kwa sababu kondo la nyuma huanza kushindwa kufanya kazi vizuri,” anasema.

Anaendelea: “Ili kuokoa maisha ya mtoto, tukishagundua hilo hutulazimu kumchoma mama sindano ya uchungu ili apate uchungu ajifungue,” anasema Dk Lulandala.

Lulandala anazidi kufafanua kwamba muda wa miezi tisa ya kujifungua ikishapita kichwa cha mtoto aliye tumboni huongezeka na kukomaa hivyo kupelekea kushindwa kuzaliwa kwa njia ya kawaida.

Chanzo: www.habarileo.co.tz