Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MSD kukabidhiwa eneo la ujenzi wa ghala Arusha

MSD Kukabidhiwa Eneo La Ujenzi Wa Ghala Arusha.jpeg MSD kukabidhiwa eneo la ujenzi wa ghala Arusha

Thu, 30 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuu wa mkoa wa Arusha John Mongella, ameuhakikishia uongozi wa Bohari ya Dawa (MSD) kuwakabidhi eneo la ujenzi wa ghala la kuhifadhia Bidhaa za Dawa kwa mkoa huo kabla ya mwezi Januari 2024 ili kurahisisha usambazaji wa dawa mkoani humo.

Mongella amesema hayo katika kikao kazi cha Bohari ya Dawa (MSD) na wateja wake kanda ya Kilimanjaro kilichofanyika mkoani Arusha na kuipongeza MSD kwa kusambaza bidhaa za Dawa nchi nzima pamoja na uwepo wa changamoto za miundombinu kwa baadhi ya maeneo.

"Mimi niahidi kwa mkoa wa Arusha, mwenzangu wa Manyara kiwanja walishakabidhi, mkoa wa Arusha mpaka tunafika mwaka mpya na sisi tutakuwa tumekabidhi kiwanja lakini pia nashauri mtaona mnawekaje kitaalamu tuweke mifumo imara ya kidigitali ambayo itasaidia sana kwenye kuimarisha mnyororo wetu wa thamani ili kuondoa changamoto nyingi zilizopo," amesema Mongella.

Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inafanya kazi kubwa kuimarisha sekta ya Afya ambayo ni sekta ya msingi kwa Watanzania na kutoa rai kwa wasimamizi taasisi kuendelea kumuunga mkono Rais ili kuhakikisha Taifa linapiga hatua kimaendeleo.

"Niseme tu kwamba Serikali ya awamu ya sita Chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, tumeona kazi kubwa iliyofanyika kwenye sekta ya Afya na Mkurugenzi Mkuu [MSD] ameonesha kwamba hata viwango vya ufanyaji kazi vimevunja rekodi za nyakati zote kwenye nchi yetu," amesema RC Mongella.

Kwa Upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Mavere Tukai amesema Bohari ya Dawa imedhamiria kupunguza kwa kiasi kikubwa uagizaji wa bidhaa za Dawa kutoka nje ikiwemo kuongeza uzalishaji nchini hali itakayopunguza uagizaji huo wa bidhaa.

"Tulikuta taasisi ina 34% tu ya bidhaa muhimu ambazo zina mikataba ya muda mrefu lakini kwa sasa tushavuka 90% na vile vile kwenye upande wa miradi maalum miradi ya ujenzi wa vituo vipya mtaona kwamba kuna mabadiliko kwa sababu ya kubadilisha mfumo mzima wa Procument [ununuzi], naomba niseme MSD ni taasisi iliyokomaa mkiangalia ukuaji wa sekta ya Afya katika miaka 10 iliyopita kwa idadi ya watu tu tumeongezeka kwa 37% kwa idadi ya vituo tumetoka vituo 5,000 hadi 7,000 na bado tunaendelea nadhani tutafika 8,000 mwezi wa saba mwakani"- amesema Tukai.

Amesema kwenye upande wa Utunzaji wa Bidhaa za Dawa umeongezeka kwa kukodisha maghala lakini tayari Bohari imeanza ujenzi kwa kuhakikisha Kanda zote zinakuwa na maghala ambayo yatatumika kutunza Bidhaa za dawa.

"Kwa sasa hivi 70% ya kanda zetu haziwezi kutunza mzigo wa zaidi ya miezi miwili na sera ya nchi inasema uwe na miezi mitano mpaka tisa, kwa hiyo tunapambana kujenga maghala ili kuhakikisha tunakuwa na viwango vya Kimataifa katika kutunza bidhaa"- ameongeza Tukai.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Manyara Dkt. Damas Kayera amesema mbali na changamoto zilizopo lakini MSD inaendelea kupiga hatua hatua kwa kuhakikisha bidhaa za Dawa zinafika kwa wakati ambazo sasa usambazaji unafanyika kila baada ya miezi miwili.

"Kwa sasa hivi bidhaa za Afya zinafanyika kila baada ya miezi miwili kwa hiyo hakuna kusubiri sana lakini tunaishukuru sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu sasa fedha zimeongezeka za kununulia vifaa, dawa na huduma za Afya kwa ujumla"- amesema Dkt. Kayera.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live