Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MATOKEO YA KIDATO CHA NNE: Kilimanjaro haishikiki, Dar yatoa ‘0’ na ‘1’ kibao

91681 Pic+matokeo MATOKEO YA KIDATO CHA NNE: Kilimanjaro haishikiki, Dar yatoa ‘0’ na ‘1’ kibao

Mon, 13 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkoa wa Kilimanjaro umeendelea kuwa kinara katika matokeo ya kidato cha nne kati ya mikoa 31, huku Kaskazini Unguja nayo ikiendelea kushika mkia kwa miaka mitatu mfululizo.

Matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2019 yaliyotangazwa wiki iliyopita na Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), yanaonyesha kuwa Kilimanjaro imeendelea kuiitesa mikoa 30 iliyobaki kwa kushika nafasi ya kwanza kwa ufaulu wa mtihani huo ambao huibua hisia za watu wengi yanapotoka. Si 2019 pekee, mkoa huo pia ulishika nafasi ya kwanza mwaka 2017 na 2018.

Katika mpangilio huo, mikoa mitano ya mwisho ni ileile kama ilivyokuwa mwaka 2018 na yote inatokea Zanzibar. Hata mwaka 2017 mikoa hiyo ilishika nafasi tano za mwisho, hali inayozua wasiwasi mkubwa wa mustakabali wa elimu katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Akizindua shule ya Mwanakwerekwe juzi, Rais John Magufuli akiwa katika ziara yake Zanzibar alisikitishwa na hali ya elimu visiwani.

“Nasikitika matokeo yanapotangazwa na kukuta shule za Zanzibar zinafuatana kuwa za mwisho. Hii ni aibu, viongozi pigeni vita hii aibu,’’ alisema.

Mikoa saba imeendelea kubaki katika kumi bora kama ilivyokuwa mwaka 2018 ukiondoa Mkoa wa Iringa ulioingia kumi bora mwaka 2019 kutoka nafasi ya 12 mwaka 2018. Mwaka huu Iringa imeshika nafasi ya tatu ikipanda kwa nafasi tisa. Mikoa mingine iliyobaki katika orodha hiyo bora ni Arusha, Njombe, Simiyu, Tabora, Kagera, Mbeya na Kigoma.

Matokeo mikoa mitatu ya juu

Matokeo hayo yanaonyesha Kilimanjaro iliyokuwa na vituo 317 vya mtihani ambavyo ni vingi kuliko mkoa wowote imepata wastani wa pointi (GPA) 3.6896 ikiwa imepanda kidogo kutoka wastani wa 3.7616 mwaka 2018. Katika matokeo hayo mkoa huo ulikuwa na wanafunzi 1,964 waliopata daraja la kwanza, la pili 3,910 , la tatu 4,756 , la nne 11, 764 huku waliofeli kwa kupata daraja sifuri wakiwa 4,395.

Arusha na Iringa ndio inayofuatia kwa ubora huku kila mkoa ukiwa na wastani wa pointi (GPA) 3.7125 na 3.7166 mtawalia.

Arusha yenye vituo 225 ina daraja la kwanza 1,429 huku Iringa yenye vituo 163 ikiwa na daraja la kwanza 726. Arusha ina sifuri 3,266 huku Iringa ikiwa na sifuri 1,333

Mkoa wa Tabora umejipambanua kwa aina yake kwa kuendelea kushika nafasi ya sita kama ilivyokuwa mwaka 2018. Ikiwa na vituo 175 na wanafunzi 476 waliopata daraja la kwanza huku 1, 637 wakipata sifuri. Mkoa mwingine uliong’ang’ania nafasi yake ya mwaka 2018 ni Morogoro iliyoshika tena nafasi ya 17 ikiwa na ufaulu wa wastani wa pointi 3.8714. Mkoa mwingine uliokataa kupanda wala kushuka ni Songwe iliyoshika nafasi ya 15 kwa miaka miwili mfululizo.

Maajabu ya Dar es Salaam

Hali bado tete kwa Mkoa wa Dar es Salaam unaotajwa kuwa na unafuu wa mazingira ya kujifunzia kuliko mikoa mingi nchini. Mwaka huu imeanguka kwa nafasi mbili hadi kuwa ya 18 kutoka nafasi ya 16 mwaka 2018. Mwaka 2017 mkoa huo pia ulishika nafasi ya 16.

Hata hivyo, mkoa huo uliokuwa na vituo 303 vya mitihani ndio wenye matokeo ya kushangaza zaidi.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na kushika nafasi ya 18 ukiachwa mbali na Kilimanjaro ndio unaoongoza kwa kuwa na wanafunzi wengi waliopata daraja la kwanza ambao ni 2,249. Kama haitoshi mshangao mwingine upo katika wanafunzi waliopata daraja sifuri, mkoa huo umeongoza kwa kuwa na wanafunzi 10,223 waliopata daraja hilo la ‘ziro’.

Mikoa mingine iliyokuwa na wanafunzi wengi zaidi waliopata sifuri ni Mwanza yenye wanafunzi 5,841 na Tanga wanafunzi 5,687. Mkoa pekee uliopata idadi ndogo ya sifuri ni Katavi iliyokuwa na wanafunzi 622 kutoka vituo vya mitihani 37.

Chanzo: mwananchi.co.tz