Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lukuvi azuia watu kuhamishwa

41901 Pic+lukuvi Lukuvi azuia watu kuhamishwa

Sat, 16 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Serikali imesitisha mpango wa kuwaondoa wakazi wa mitaa minne ya Morogoro waliovamia maeneo ya hifadhi ya Bwawa la Mindu na kuanzisha makazi na shughuli za kibinadamu ikiwamo kilimo na uchimbaji wa madini.

Mpango wa kuwaondoa ulipangwa kuanza wiki ijayo ukitekelezwa kwa ushirikiano kati ya uongozi wa Mkoa wa Morogoro na Bodi ya Maji ya Bonde la Wami Ruvu ukilenga kukabiliana na uharibifu wa maji ya bwawa hilo ambalo linachangia asilimia 80 ya maji yote yanayotumika katika mji wa Morogoro.

Jana, mawaziri wanane wakiongozwa na William Lukuvi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi walitembelea bwawa hilo na baada ya ukaguzi walitoa tamko kwamba mpango huo usitishwe kwanza wakati Serikali ikiendelea kuangalia njia nyingine bora ya kukabiliana na hali hiyo.

Alisema timu ya mawaziri wanane imeundwa kupitia maeneo yenye migogoro ya kuingiliana kati ya makazi ya watu, shughuli za kibinadamu na hifadhi.

Lukuvi alieleza kuwa mgogoro unaoendelea katika bwawa hilo ni eneo mojawapo wanalolifanyia kazi ambalo watakiwa kutoa ripoti yake baada ya siku 30.

“Tumesikia mlitaka kuwatoa, sasa tunasema msifanye chochote hadi pale mtakapopata maelekezo kutoka kwa waziri mwenye sekta,” alisema Waziri Lukuvi.

“Tumepewa jukumu hilo na Rais (John Magufuli) kumshauri namna ya kukabiliana na migogoro inayotokana na uvamizi hasa katika maeneo ya hifadhi na maliasili, sasa tumesikia, tunaenda kufanyia kazi,” alisema Lukuvi ambaye ni mwenyekiti wa timu hiyo.

Awali, ofisa wa maji wa Bonde la Wami Ruvu, Simon Ngonyani alisema uwepo wa makazi ya watu ndani ya mita 500 kutoka lilipo bwawa hilo unasababisha uharibifu mkubwa wa maji.

Alisema shughuli za kilimo zinasababisha kemikali zinazotokana na mbolea kuchafua maji pamoja na tope kuingia bwawani.

Sanjari na hilo, alisema uchimbaji wa madini unaofanyika unasababisha kemikali ya zebaki kuingia kwenye maji jambo ambalo linaweza kuleta athari.

“Ukiacha yote hayo sababu kubwa zaidi tunayotaka hawa watu waondoke ni usalama wao, ikitokea bwawa likapasuka madhara yatakayowapata ni makubwa mno.”

Katika eneo hilo kuna watu wapatao 133 wanaomiliki mashamba 261 wakisema hawawezi kuondoka kwa kuwa hawana pa kwenda.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Stephen Kebwe alisema Serikali haitawafidia tena wakazi hao kwa kuwa tayari wahusika walishalipwa nao wameuza kwa wengine.

Mawaziri wengine walioongozana na Lukuvi ni; Luhaga Mpina (Mifugo na Uvuvi), Profesa Makame Mbarawa (Maji), Selemani Jafo (Tamisemi), Dk Hamis Kigwangalla (Maliasili na Utalii), Dk Hussein Mwinyi (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa), Omar Mgumba (Naibu Waziri wa Kilimo), na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais (Muungano na Mazingira) Mussa Sima.



Chanzo: mwananchi.co.tz