Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lukuvi azitaka halmashauri kutenga bajeti ya kujenga nyumba

17813 Pic+lukuv TanzaniaWeb

Mon, 17 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Bunda. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amezitaka halmashauri zote nchini zenye uhitaji wa nyumba za watumishi kutenga bajeti ili waweze kujengewa nyumba hizo na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Waziri Lukuvi ameyasema hayo leo Septemba 17, 2018 mjini Bunda mkoani Mara alipokuwa akijibu ombi la mkuu wa wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili aliyemuomba waziri huyo kuruhusu NHC kuingia mkataba na wilaya yake kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za watumishi katika wilaya hiyo.

Waziri Lukuvi alisema shirika hilo lipo tayari kujenga nyumba muda wowote  endapo halmashauri husika itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi huo tofauti na zamani ambapo NHC ilikuwa ikijenga nyumba kabla ya kuingia mkataba na halmashauri husika hali iliyosababisha nyumba nyingi kuchukua muda mrefu bila kununuliwa.

"Shirika linajiendesha kibiashara na tunakopa fedha benki kwa hiyo ni vema mkatenga fedha kabisa kuliko kujenga halafu tukaanza kudhulumiana au tukajenga tukaanza kutafuta wateja," alisema Lukuvi.

Awali, mkuu wa wilaya ya Bunda, Bupilipili amemwambia Waziri Lukuvi kuwa watumishi katika wilaya hiyo hawana nyumba za kutosha hivyo kuomba shirika la nyumba kuwajengea nyumba kwa mkataba maalum.

"Mheshimiwa waziri kwa vile sisi tuna ardhi, tunaomba shirika litujengee nyumba tuingie mkataba namna ya kulipana ili tuweze kuondokana na tatizo la ukosefu wa nyumba za watumishi," alisema Bupilipili.

Chanzo: mwananchi.co.tz