Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lukuvi awapa wananchi hekta 300

24669 Pic+lukuvi TanzaniaWeb

Wed, 31 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Same. Baada ya kilio cha wananchi kukosa ardhi huku maeneo makubwa yakimilikiwa na wawekezaji bila tija, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ameingilia kati na kuamuru wapewe hekta 300.

Akizungumza na wanavijiji vitatu vya Msufini, Gonja Mperani na Ndungu juzi, Lukuvi aliwaeleza kuwa moja ya kazi ya Serikali ni kuondoa kero, kulinda wawekezaji na kutetea wanyonge.

Awali, wenyeviti wa vijiji vya Msufini, Gonja Mperani na Ndungu waliiomba Serikali kuwapatia hekta 100 kila kijiji ili ziwasaidie katika shughuli zao. Mwenyekiti wa Msufini, Omar Mganga alimweleza waziri kuwa kijiji chake kina uhaba wa ardhi jambo linalosababisha wananchi kukosa maeneo ya makazi, makaburi.

Waziri Lukuvi alifafanua kuwa jukumu la Serikali si kufukuza wawekezaji bali kuwa na wawekezaji wenye tija, watakaoleta teknolojia mpya na kuongeza pato la taifa.

Katika kutatua mgogoro huo, Lukuvi aliamuru vijiji hivyo kupatiwa hekta 300 ambazo zitamegwa kutoka eneo lenye ukubwa wa hekta 1,230 linalomikiwa na kampuni ya LM Investments Ltd.

Lukuvi alisema kati ya hekta hizo, 71 ni zile zilizoongezwa tofauti na makubaliano ya umilikishwaji mwaka 1998 na nyingine zitatoka ndani ya eneo linalomilikiwa na kampuni hiyo hali iliyozusha mlipuko wa shangwe kwa wananchi.

Waziri aliamuagiza mkuu wa Wilaya ya Same na ofisi ya kamishna msaidizi Kanda ya Kaskazini kufanya uhakiki upya wa eneo hilo na kwamba kazi hiyo ifanyike ndani ya miezi miwili, huku akiwataka viongozi kuheshimu mipaka itakayowekwa baada ya zoezi la kugawa maeneo kukamilika.

Bodi haijaachwa salama

Lukuvi aliijia juu Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB) kwa kushindwa kusimamia kampuni zinazozalisha zao hilo huku mashamba mengi kati ya hayo uendeshaji wake ukiwa hauna tija, hayatoi ajira za kutosha kwa wananchi waliopo jirani na kuikosesha Serikali mapato.

Alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita alipozungumza na uongozi wa kampuni ya kuzalisha mkonge ya LM Investments Ltd katika kijiji cha Ndungu wilayani Same mkoani Kilimanjaro.

“Kama bodi wameshindwa kuchukua hatua kwa wasiofanya vizuri basi wizara tutafanya ukaguzi kwa mashamba yote tubaini wasiofanya vizuri tuwanyang’anye tuwapatie wengine wenye uwezo,” alisema.

Kauli hiyo inafuatia kutoridhishwa na uendeshaji wa shamba la mkonge la Ndungu lenye ukubwa wa hekta 1,230 linalomilikiwa na LM Investments Ltd.

Awali, naibu mkurugenzi mtendaji wa LM Investments Ltd, Allan Chellangwa alisema shamba hilo limekuwa likizalisha wastani wa tani 30 kwa mwezi na lengo ni kuzalisha tani 50, limeajiri wafanyakazi 24.

Chanzo: mwananchi.co.tz