Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lukuvi atumia saa saba kusikiliza kero 400 za ardhi

32310 Pic+lukuvi Tanzania Web Photo

Wed, 19 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kama ni wingi wa vilio vinavyowasibu wananchi, basi ardhi ni kero kubwa kwa wengi.

Kila anakokwenda, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amekuwa akikutana nazo, na mara zote imeibuka mikasa ya ajabu juu ya ardhi kwenye mikutano yake.

Akiwa mkoani Mara, miezi miwili iliyopita kuna siku alisikiliza karibu kero 1,000, kisha akakutana nazo nyingi mkoani Tabora alikolazimika kuzisikiliza hadi usiku.

Hata juzi alipokuwa wilayani Ilala jijini hapa ilikuwa ni hivyo, kwani ilimchukua zaidi ya saa saba kuanzia saa 8:06 mchana hadi saa 02:12 usiku kusikiliza kero za migogoro ya ardhi, mashamba na nyumba zaidi ya 400 za wakazi wa wilaya hiyo kwenye viwanja vya Kampala, Gongolamboto.

Lukuvi yuko mkoani Dar es Salaam akiendelea na ziara ya siku tano aliyoianza juzi kusikiliza kero za wananchi zinazohusu migogoro ya ardhi iliyopewa jina la “Funguka kwa Waziri”.

Kabla ya kusikiliza kero hizo, Lukuvi aliwataka wananchi kutimiza wajibu kabla ya kudai haki ikiwa ni pamoja na kulipa kodi ya ardhi na majengo wanayomiliki. Alisema ifikapo Juni mwakani, viwanja na nyumba ambavyo havijalipiwa kodi vitataifishwa na kupigwa mnada.

Alifafanua kuwa kabla ya hatua hiyo Wizara ya Ardhi itafanya ukaguzi wa makazi ambayo hajalipiwa kuanzia Machi, 2019.

Waziri huyo alisema wametoa muda wa kulipa bila adhabu kuwa ni Desemba na Januari na wale ambao watakuwa hawajafanya hivyo hadi Juni viwanja au nyumba ambavyo havijalipiwa vitapigwa mnada.

“Hatuna mzaha ndiyo maana tumekuja huku mlipo kutatua kero zenu, lakini kabla hamjadai haki timizeni wajibu wenu, ambaye atakutwa hajalipa kodi kwa kipindi hicho chote tutapiga mnada mali yake ili tufidie malipo aliyolimbikiza,” alisema.

Alisema anatambua ugumu wa kazi iliyo mbele yake kwa sababu Dar es Salaam inaongoza kwa kuwa na migogoro mingi ya ardhi ambayo ni asilimia 80 ya migogoro yote nchini.

Alisema kwa kulitambua hilo, wamekuwa wakitafuta mbinu mbadala za kukabiliana na hali hiyo ikiwamo ya kuanzisha kadi za kielektroniki na urasimishaji maeneo yasiyo rasmi.

“Wajanja wa mjini wanaoishi kwa kuiba ardhi wanatumia hayo maeneo ambayo hayajarasimishwa kwa kuvamia na kujimilikisha huku watumishi wa wizara wasio waaminifu wakitoa hati bandia” alisema Lukuvi.

Miongoni mwa kero alizosikiliza ni pamoja na ya mzee Omari Shomvi Nyawili aliyedai kudhulumiwa hati kwa udanganyifu.

Akizungumza kwa shida mbele ya waziri kutokana na utu uzima, mzee huyo alisema alikuwa anauza nyumba yake iliyokuwa Tandale kwa Sh65 milioni, lakini mnunuzi alimpa Sh10 milioni na kuchukua hati yake kwa madai ya kwenda kuhakiki Wizara ya Ardhi na tangu hapo ni mwaka mmoja umepita hajairudisha na akipigiwa simu hapokei.

Kutokana na malalamiko hayo, Lukuvi alimpigia simu palepale mtu huyo lakini hakupokea na kumwagiza Kamanda wa Polisi Kinondoni, Murilo Jumanne kumfikisha kwenye mkutano wa Kinondoni ili akatoe majibu kwa nini hajamlipa na wala kurudisha hati ya nyumba ya mzee huyo.



Chanzo: mwananchi.co.tz