Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lukuvi ashtukia wapigaji Morogoro

58332 Pic+lukuvi

Mon, 20 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kilosa. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema watapitia upya mashamba yote yaliyofutwa na Rais wilayani hapa mkoa wa Morogoro.

Lukuvi alisema hayo juzi akiwa katika kata ya Chanzulu tarafa ya Kimamba wilayani Kilosa alipozungumza na wananchi, alipokwenda kutatua mgogoro wa ardhi.

Alisema kuna mashamba yaliyofutwa na Rais maeneo mbalimbali lakini hayajawekewa utaratibu wa kutumiwa, hivyo kutoa fursa kwa wajanja kujigawiwa na mengine kuyauza bila kufuata utaratibu.

Waziri huyo alisema katika kuhakikisha mashamba yote yaliyofutwa wilayani hapa umezuka mgogoro baina ya wananchi na wamiliki, hivyo Serikali imeamua kupeleka timu kuyahakiki.

Alisema timu hiyo inajumuisha kamishna wa ardhi, kaimu mkurugenzi upimaji na ramani, mthamini mkuu wa Serikali, kamishna msaidizi wa ardhi Kanda ya Kati na wataalamu kutoka idara za mipango miji wizarani.

Lukuvi alisema uamuzi huo unalenga kumaliza migogoro ya ardhi wilayani hapa, baada ya kubaini ofisi za wilaya na mkoa zimeshindwa kutatua mgogoro huku viongozi wake wakituhumiwa.

Pia Soma

“Tutayapitia mashamba yote 15 yaliyofutwa na Rais kujua kilichomo ndani yake na timu ya uhakiki niliyokuja nayo itanilitea mapendekezo namna ya kuyatumia na mengine watapewa wanaostahili si kila mtu,” alisema.

Naye mkuu wa idara ya ardhi, maliasili na mazingira wa halmashauri ya Kilosa, Ibrahim Mndembo alisema mashamba 25 yenye ukubwa wa eka 23,596 maeneo ya Msowero, Magole na Chanzulu katika wilaya ya Iringa Kilosa yamebatilishwa umiliki.

Mashamba yenye mgogoro na wananchi ni Noble Agriculture Enterprises, Magereza, Mbigiri na Mabwegere, Chadulu Estate, Shamba la Swai na Mauzi Estate Malangali.

Mengine kufutiwa umiliki

Waziri Lukuvi alisema mashamba yote yaliyopo wilayani Kilosa yatahakikiwa ili kubaini yasiyoendelezwa yafutiwe umiliki.

Akizungumza na wananchi wa Mvumi juzi, Lukuvi alisema uamuzi huo unatokana na uwapo wa dalili za upendeleo wakati wa kupendekeza mashamba 15 yaliyofutwa na Rais.

Lukuvi alisema Kilosa ina mashamba 183 na yote yatafanyiwa uhakiki na timu ya wataalamu 15 kutoka wizarani, kubaini yasiyoendelezwa na kuwasilisha mapendekezo kwake.

Awali, Mndembo alisema tayari mashamba 15 yamefutiwa umiliki.

Chanzo: mwananchi.co.tz