Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lukuvi aingilia kati mgogoro wa ardhi Monduli

28536 Lukuvi+pic TanzaniaWeb

Sun, 25 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Monduli. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, ametuma timu maalum ya maofisa ardhi mkoa wa Arusha kufuatilia tena mgogoro wa ardhi, kijiji cha Eng'arooji Kata ya Lepurko wilayani Monduli mkoani Arusha .

Katika kijiji hicho, wiki iliyopita wananchi kupitia mkutano mkuu waliamua wafugaji wanne kunyang'anywa ekari 1,215 za ardhi na kuzigawanya kwa wasio na ardhi na wafugaji hao kuachiwa ekari 50 kila mmoja.

Lukuvi alitangaza jana Alhamisi kuunda kamati, hiyo baada ya kukutana na viongozi wa Serikali ya kijiji cha Eng'arooji, wafugaji wanne waliokuwa wanamilikishwa ardhi na maafisa wa ardhi na sekretarieti ya mkoa wa Arusha.

Waziri Lukuvi ameipa kamati hiyo siku 14 kupima kijiji hicho, ikiwemo mashamba ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na wananchi kumilikiwa na wafugaji hao kinyume cha sheria na kumpa taarifa.

Wafugaji walionyang'anywa ardhi hiyo ni Paulo Ndari aliyekuwa anamiliki ekari 716, Lekashu Ngeney ekari 301, Sarimu Orkoskos ekari 268 na Metui Onyetu ekari 130, wanadaiwa walimilikishwa ardhi hiyo kinyume cha sheria.

Mbunge wa Monduli, (CCM) Julius Kalanga amesema wakazi wa Monduli wana imani na kamati hiyo ya waziri itafanya kazi nzuri na kuwezesha kutatuliwa mgogoro huu.

"Tuna imani na Waziri Lukuvi atamaliza mgogoro huu, wakati wa kampeni zangu alikuja Monduli na alipata malalamiko ya mgogoro huu na alifanya uamuzi wa kusitisha hati," alisema.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Ngalama Mapena alisema wana imani mgogoro huo sasa utafikia mwisho na kuepusha maafa katika kijiji chake.

"Wananchi walifanya uamuzi na sasa waziri anataka kujiridhisha  kabla ya kutoa uamuzi," alisema.

Hata hivyo, wafugaji hao wakiongozwa na mmoja wa wamiliki wa ardhi hiyo, Paulo Ndari wamepinga uamuzi wa kunyang'anywa ardhi hiyo na kudai wao walimilikishwa kimila ardhi hiyo.

Mapema Septemba akiwa katika mikutano ya kampeni katika jimbo la Monduli, Waziri Lukuvi alitangaza kusitishwa hati za umiliki wa ardhi wananchi hao ili kupisha uchunguzi.

Waziri Lukuvi licha ya kusitisha hatimiliki ya wafugaji hao, pia aliagiza kusimamishwa kazi, ofisa ardhi wilaya ya Monduli, Kitundu Mkumbo kwa kutoa hati hizo kinyume cha sheria.



Chanzo: mwananchi.co.tz