Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lukuvi afunga ofisi nzima, ageukia wamiliki viwanja

Fri, 30 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri wa Ardhi, William Lukuvi jana alifunga ofisi za ardhi na masijala za Jiji la Dar es Salaam, akisema anafunga mtambo wa kufyatua migogoro ya ardhi.

Waziri Lukuvi pia amewaonya wamiliki katika Mradi wa Viwanja 20,000 kukaa chonjo kwa kuwa wanaweza kunyang’anywa, huku akiagiza kuanza kwa msako wa watu waliotelekeza hati 6,000 za umiliki wa viwanja zilizotolewa na wizara yake takribani miaka 20 iliyopita.

Lakini, moto ulikuwa ofisi ya ardhi ya Jiji la Dar es Salaam ambako Waziri Lukuvi alitaka maofisa hao wakusanye nyaraka za ofisi yao na kuhamia wizarani kwa kuwa hawana cha kufanya eneo hilo.

“Mnajua kwa muda mrefu nimekuwa nikipambana na migogoro ya ardhi nchini, leo imefika tamati. Nimeshagundua chanzo chake kinatokea hapa. Nazifunga hizi ofisi,” alisema Waziri Lukuvi.

“Hizi ofisi zinatoa hati zisizotambulika kwa kisingizio cha ofa. Mtu yeyote mwenye ofa ya kiwanja na ina muhuri wa jiji haitambuliki. Aende kwa kamishna wa ardhi wa wilaya ilikotolewa ofa hiyo kwa ajili ya maelekezo ya jinsi ya kupata hati halisi, maofisa msipokee tena ofa hizo.”

Lukuvi ambaye alifika ofisi za jiji akiambatana na maofisa wa wizara yake pamoja na waandishi wa habari, alisema jiji halina ardhi, halipangi, halipimi na wala halimilikishi lakini linaendelea kutoa ofa za ardhi ambazo zinaisumbua wizara yake.

Alisema shughuli zote za ardhi zitafanywa na wilaya tano za Dar es Salaam na kanda, hivyo hakukuwa na sababu ya maofisa hao kuwa ofisi ya jiji.

Maofisa hao walijaribu kujitetea, lakini Waziri Lukuvi hakutaka kuwasikiliza akiwaambia watafanya hivyo wizarani.

Mkurugenzi wa Jiji, Spora Liana alisema kumekuwa na matumizi mabaya ya ofa kwa kuwa awali kulikuwa hakuna halmashauri na baada ya kuanzishwa, wajanja wamekuwa wakitumia maofisa ardhi wa jiji kuwatengenezea ofa ambazo huwekwa tarehe za zamani na hivyo kufanikisha umikishwaji usio halali.

Ofa ni nyaraka zilizokuwa zikitolewa kama sehemu ya mchakato wa kumilikishwa ardhi kabla ya kupata hati, lakini ilibainika baadaye zilikuwa zikitumika kumilikisha kinyemela watu walioongea vizuri na maofisa ardhi na kuwapora wanyonge haki zao.

Lukuvi alisema kwa sasa wanaendelea kukusanya taarifa na wakishaingia rasmi kwenye mfumo wa digitali, ofisi za ardhi za mikoa hazitatambulika tena na kuanzia sasa maombi yote yatatoka wilayani kwenda kwa kamishna wa ardhi wa wilaya husika.

“Kuna watu wamekaa mkao wa kula kazi yao kuchapisha ofa za jiji, nilishatoa miaka miwili watu wenye ofa hizi wazibadilishe kupitia kwa maofisa wa ardhi wa wilaya. Kuanzia sasa imekula kwao hatuzitambui tena,” alisema Lukuvi.

“Tunatoa hati moja kwa moja hakuna ofa. Nimeamua kufunga ofisi za ardhi za jiji na watendaji wote wataripoti wizarani.”

Mradi wa viwanja 20,000

Kuhusu walionunua viwanja kwenye Mradi wa Viwanja 20,000, Lukuvi alisema wote ambao hawajaviendeleza mwisho wa kuvimiliki ni Desemba.

Mwezi Juni, wizara hiyo ilitoa wiki mbili kwa walionunua viwanja hivyo kuviendeleza na kwamba ingeanza kukagua ili watakaobainika wachukuliwe hatua.

Jana Lukuvi alisema atawasamehe wale ambao watakuwa angalau wameweka uzio wa matofali na siyo wa maua au waya.

Mradi huo ulihusisha viwanja vilivyoko Bunju, Mpiji, Toangoma, Mwanagati, Kibada, Gezaulole, Mwongozo, Mbweni, Mbweni Malindi, Mbweni JKT na Kibada.

“Nilichogundua baadhi ya viwanja viliwekwa majina bandia, havina wamiliki na wengine wamesahau,” alisema.

“Nimewaita hawa maofisa wa wizara ili niwape maagizo ya mwisho, wafanye uchunguzi kwa yeyote aliyenunua kiwanja hajajenga hata ukuta, taratibu za kuchukua kiwanja chake zianze mara moja.

“Wale wachache waliojenga hawakai kwa raha kuna watu wanawavamia na kuwasumbua, hivyo watakwenda kuvifuatilia na kujua wamiliki ni kina nani. Inawezekana maofisa ardhi walivichukua na kuvitelekeza.”

Katika hatua nyingine, waziri huyo aliagiza msako wa kuwatambua wenye hati 6,000 waliozitelekeza katika wizara hiyo.

Huku akionyesha rundo la hati hizo kwenye makabati wizarani hapo, alisema zipo zilizotelekezwa kwa zaidi ya miaka 20.



Chanzo: mwananchi.co.tz