Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lukuvi: Dar itapangwa upya

00c02068b64b940093c5d3a6513814ab Lukuvi: Dar itapangwa upya

Sat, 17 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKOA wa Dar es Salaam unatarajiwa kufumuliwa, kupangwa na kuwa katika mwonekano mpya kutokana na Ramani ya Mpango wa Mji huo kukamilika huku ikitarajiwa kuzinduliwa karibuni.

Aidha, Serikali imesema inaanza uhakiki wa umiliki wa ardhi nchini kwa kutumia vitambulisho vya uraia kubaini viwanja hewa na raia wa kigeni wanaomiliki ardhi.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alisema hayo kwenye Kikao Kazi na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makala, wakuu wa wilaya, wakurugenzi na watendaji wakuu serikalini kuhusu masuala ya ardhi, ikiwamo kukabiliana na migogoro ya ardhi.

Dar mpya

Lukuvi alisema Mpango Mji huo utakaozinduliwa hivi karibuni utatoa nafasi ya kubadili mpango mji wa mwisho ambao uliondaliwa mwaka 1979, hivyo kuwa na muundo na mwonekano mpya kwa kujengwa miji ya kisasa.

Alisema mpango huo mpya umekamilika hivyo ni vema Mkuu wa Mkoa na wakuu wa wilaya wakaandaa siku ambayo watakaa na kuangalia mkoa ulivyopangwa pamoja na kupanga siku ya uzinduzi rasmi kabla ya kuanza kuendeleza mkoa huo kutumia mpango huo mpya.

Waziri Lukuvi alisema katika mpango huo mpya ulioandaliwa na wataalamu kutoka vyuo vikuu nchini, unahuisha uendelezaji wa masuala kadhaa ikiwemo baadhi ya maeneo ambayo yalikuwa hayaruhusiwi kujengwa maghorofa lakini sasa yameruhusiwa.

Alitaja maeneo hayo kuwa ni pamoja na Manzese na Magomeni.

“Hili litatoa nafasi kwa wawekezaji kujenga majengo ya kisasa ambayo yana maghorofa na kuwezesha wananchi kukaa huku kukifanyika uwekezaji wa aina mbalimbali pamoja na masuala mengine yaliyopo katika mpango huu,” alisema.

Alisema kutaanzishwa mji mpya ili kupunguza msongamano katikati ya miji pamoja na maeneo mengine kujengwa majengo ya kisasa.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makala alisema baada ya kutaarifiwa kukamilika kwa Mpango Mji mpya wataandaa siku maalumu kufanya uzinduzi katika hafla kubwa itakayokuwa ya kihistoria.

“Katika siku hiyo ya uzinduzi itakayofanyika hivi karibuni, tutakutana na kuweka mikakati ya kupanga baada ya watendaji wa mkoa kukutana na wataalamu na kuangalia jinsi Master Plan hiyo ilivyo,” alisema.

Uhakiki ardhi

Akizungumzia uhakiki ili wamiliki wote wa ardhi kusajiliwa kwa kutumia vitambulisho vya taifa, Lukuvi alisema utasaidia kutambua viwanja hewa, wadanganyifu na wamiliki wa ardhi wasio raia.

Anasema hii inatokana na miaka ya nyuma wananchi kumilikishwa ardhi kwa kutumia vyeti vya kuzaliwa na namba ya Sanduku La Posta.

“Kwa sasa tutasajili namba za simu zitakazosaidia katika kukumbusha ulipaji wa kodi na masuala mengine kutokana na wamiliki wengi kuwa na namba za simu. Napenda kuwahakikishia wananchi katika uhakiki huu hakuna atakayenyanganywa kiwanja,” alisema.

Waziri Lukuvi alibainisha kuwa sheria za nchi hazina ukomo wa umiliki wa ardhi hivyo wale wenye viwanja vingi ambao waliviandikisha kwa majina tofauti kwa kuhofia kujulikana, sasa watatumia majina yanayosomeka katika vitambulisho vya uraia.

Alisema uhakiki utabaini viwanja ambavyo havina wamiliki vikiwamo vya baadhi ya maofisa wa ardhi ambao zamani walijimilikisha viwanja vingi lakini kabla hawajataarifu familia zao wakafariki dunia.

Alisema kuna viwanja ambavyo havifahamiki wamiliki wake katika maeneo mbalimbali pamoja na vile vya miradi ya viwanja 20,000 vilivyopimwa na wizara.

Chanzo: www.habarileo.co.tz